Maana ya historia
Historia ni mfululizo wa habari za mambo yaliyotokea pamoja na sababu zake. Binadamu anaziandika ili kuelewa maisha yake, yaani ametokea wapi, amepata mafanikio gani na matatizo gani. Historia inatufundisha kuishi: kumbukumbu za mambo ya zamani (vita, uhuru, viongozi na mengineyo) zinatuwezesha kuendelea vizuri zaidi. Lakini ni muhimu zaidi kujua mambo makuu aliyoyatenda Mungu ili kutuokoa. Dini ya Uyahudi na ya Ukristo ni dini zinazotegemea historia kuliko maumbile: Mungu hatazamwi kama Muumba tu, bali zaidi kama Mwokozi.Maana ya wokovu
Wokovu ni kazi ya Mungu kwa ajili yetu (1Tim 2:4; 2Tim 1:9-10). Sisi hatuwezi kujikomboa, lakini Mungu ana nguvu kuliko shetani na mabaya yote, naye anatuhurumia sisi maskini (Kol 1:13-14). Alifanya nini ili kutuokoa? Ndiyo historia ya wokovu. Wapo walioiandika katika Biblia ili tusadiki na kuishi upya (1Pet 1:10-12). Humo mtu hatazamwi kama nafsi ya peke yake tu, bali zaidi kama mtu wa taifa lake; hivyo Mungu anatangazwa kuwa hashughulikii wokovu wa mtu binafsi tu, bali wa mataifa mazima pia, kuanzia lile la Israeli. Aliyowatendea wao ni hasa kuwatoa utumwani Misri, kuwapa agano na masharti yake li awafanye taifa huru katika nchi bora. Waisraeli walijenga imani yao juu ya hayo mang’amuzi ya msingi ya wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, halafu wakajikumbusha kwamba alikuwa ameshawaahidia mababu wao baraka kama hizo. Hatimaye tu walitafakari juu ya asili ya watu na ya ulimwengu, wakaelewa kuwa Mungu aliweza kuwaokoa kwa sababu ndiye aliyeumba vyote: hakuna wa kushindana naye na wa kuzuia mpango wake kwa ajili ya watu. Kwa Wakristo tukio kuu lililo msingi wa imani ni ufufuko wa Yesu, aliyetoka kaburini mzima na mtukufu, wa kwanza kati ya umati, akaingia katika nchi ya walio hai kweli.Imani kuhusu Biblia
Wakristo wanasadiki Biblia imeandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu (2Pet 1.20-21; 2Tim 3:16): ndiyo sababu wanaiheshimu sana. Lakini habari zake hazifuati mpangilio wa tarehe. Wapo wataalamu waliozipanga kwa utaratibu huo unaotupendeza zaidi siku hizi: wamejitahidi kuelewa tarehe ya matukio na ya maandiko yote ili kuyapanga moja baada ya lingine kuanzia ya zamani za kale hadi maisha ya Yesu na ya Mitume wake. Lakini tukumbuke daima kwamba lengo la Biblia si kueleza sayansi, jiografia wala historia, bali ni kufundisha kwa ukweli njia ya wokovu. Taarifa nyingine zinategemea ujuzi wa mtu aliyeandika na mtindo alioutumia: sheria, taratibu za ibada, nasaba, ufafanuzi wa majina, maneno matakatifu ya mahali fulani, baraka, hadithi, simulizi, historia halisi n.k.Sehemu kuu mbili za Biblia ni Agano la Kale na Agano Jipya (2Kor 3:10; Eb 8:13). La Kale limeandikwa kabla ya Yesu, Jipya baada yake. Hata hivyo Agano la Kale lina utabiri mwingi juu ya Yesu (Lk 24:27,44), na Agano Jipya linarudia na kufafanua habari nyingi za kale: hivyo tunatakiwa kusoma daima Agano la Kale kwa mwanga wa Agano Jipya, na kutafuta katika habari za kale mifano inayotusaidia kuelewa mambo ya Yesu na Kanisa (1Kor 10:11; Kol 2:17). Kwa kuwa ufunuo wa Mungu ulifanyika hatua kwa hatua hata ukakamilishwa na Yesu (Eb 1:1-2), hatuwezi kutegemea dondoo moja tu kuhusu jambo fulani, bali tuzingatie jambo hilo lilivyoozungumziwa tangu mwanzo hadi mwisho wa ufunuo. Tunahitaji kujua Biblia nzima ili kuelewa jinsi Mungu alivyo, alivyotuokoa na anavyotaka tuishi.
Vitabu vya Biblia ni 73: yaani 46 katika Agano la Kale na 27 katika Agano Jipya. Ndivyo vilivyokubaliwa na Kanisa Katoliki kuwa ni Neno la Mungu. Waprotestanti wengi wanakataa vitabu 7 vya Agano la Kale (pamoja na sehemu chache za vingine): hivyo Biblia yao inavyo 66 tu.
Mgawanyo wa vitabu hivyo si muhimu, mradi tusiongeze wala kupunguza neno. Kwa kawaida vinapangwa kwa kuzingatia vinaleta habari za namna gani. Hivyo katika Agano la Kale yanatofautishwa makundi manne: Torati (yaani sheria), vitabu vya historia ya Israeli, vitabu vya manabii (waliotumwa na Mungu ili kuwaonya na kuwafariji Waisraeli), na vitabu vya hekima (vyenye nyimbo, mashairi, mithali n.k.). Katika Agano Jipya tuna vitabu 5 vya historia (yaani Injili 4 na Matendo ya Mitume), barua 21 za Mitume na kitabu kimoja tu cha kinabii (Ufunuo).
Lugha asili ziko tatu, yaani Biblia imeandikwa sehemusehemu kwa Kiyahudi, Kiaramu (ndiyo lugha ya Yesu), na Kiyunani (yaani Kigiriki cha zamani). Ila Agano Jipya lote limeandikwa kwa Kiyunani ambacho zamani za Yesu kilikuwa lugha ya kimataifa. Kutoka lugha hizo wataalamu wanaendelea kutafsiri Biblia katika lugha yoyote ili Neno la Mungu liwaelee watu wote. Kati ya tafsiri zote, mbili za zamani zina sifa za pekee, yaani tafsiri ya LXX (kwa Kigiriki "Septuaginta", yaani sabini: ni Agano Kale kwa lugha ya Kiyunani), na ya Vulgata (Biblia nzima kwa Kilatini).
Maelezo ya Kanisa yanahitajika kwa sababu: kwanza mwenyewe sielewi maandiko hayo yameandikwa na nani, lini, wapi, kwa lengo lipi na katika mazingira ya namna gani. Hasa Roho Mtakatifu hakunipa Biblia peke yangu, bali ndani ya taifa lote la Mungu. Hivyo sina haki ya kuifafanua ninavyotaka. Wasio na elimu na msimamo wanapotosha Biblia na kupotea (2Pet 3:16).
Agano la Kale
Vitabu vya Agano la Kale
Mwanzo Kutoka Walawi Hesabu Kumbukumbu Yoshua Waamuzi Ruthu Samueli I Samueli II Wafalme I Wafalme II Mambo ya Nyakati I Mambo ya Nyakati
II Ezra Nehemia TobitiDK YudithiDK Esta Wamakabayo
IDK Wamakabayo
IIDK Yobu Zaburi Methali Mhubiri Hekima DK SiraDK Wimbo Bora Isaya Yeremia Maombolezo BarukuDK Ezekieli Danieli Hosea Yoeli Amosi Obadia Yona Mika Nahumu Habakuki Sefania Hagai Zekaria Malaki - Alama ya
DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote
ya Biblia.[hariri] Vitabu vitano vya Torati
Vitabu vya kwanza vya Biblia (Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati) vinaunda kwa pamoja Torati (kwa Kiyahudi “fundisho”, yaani “sheria”). Mgawanyo wa kawaida wa Kiyahudi wa vitabu vya Biblia katika makundi matatu (Torati, Manabii na Maandishi) unaonyesha jinsi vitabu vitano vya kwanza vinavyotazamwa kuwa kitu kimoja, tena kiini cha Agano la Kale lote. Ajabu la Torati ni jinsi inavyounganisha mambo mbalimbali: ibada kwa Mungu pekee, ahadi zake, matakwa yake, uasi wa binadamu na ukombozi wa Kimungu, wito wa kujali mwanzo wa taifa la Mungu.Humo tunakuta muhtasari wa historia kuanzia uumbaji wa ulimwengu hadi kifo cha Musa: historia ya asili (Mwa 1-11), kipindi cha mababu (Mwa 12-36), simulizi la Yosefu (Mwa 37-50), ukombozi toka Misri na safari kwenye Sinai (Kut 1-18), toleo la sheria mlimani huko (Kut 19 – Hes 10), safari hadi mabonde ya Moabu (Hes 10-36) na nyongeza (Kumb 1-34).
Zamani Musa alidhaniwa kuwa mwandishi wa vitabu hivyo vyote. Siku hizi wataalamu wamethibitisha kuwa ndiye asili ya kiini cha sheria za Israeli, lakini vitabu hivyo viliandikwa katika kipindi kirefu hadi mwaka 400 hivi K.K. Ndiyo sababu katika sheria za vitabu hivyo yanaonekana mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika karne hadi karne, k.mf. kuhusu Pasaka na umoja wa hekalu. Waliohusika na uandishi ni watu wengi wa Israeli Kaskazini na Kusini. Hasa yameainishwa mapokeo manne tofauti: J (yaliyoandikwa katika karne X K.K. kwa kumuita Mungu YHWH), E (ya karne IX K.K. yanayomuita Elohim), D (yanayotawala Kumbukumbu ya Torati: ni ya karne VII K.K.) na P (yaani ya kikuhani kwa kuwa yanajali sana ibada: ni ya karne VI K.K.). Hayo ya mwisho yalitumika kama fremu ya mapokeo hayo yote ili kuunganisha Torati nzima katika karne V K.K. Hivyo Torati inatunza matukio ya msingi na imani ya taifa la Israeli jinsi ilivyozidi kukomaa baada ya Musa.
Uumbaji
Uumbaji unasimuliwa katika sura mbili za kwanza za Mwanzo. Kama vile sehemu mbalimbali za Biblia, kitabu hicho kilitungwa kwa kushona pamoja maandishi tofauti. Ndiyo sababu tunakuta masimulizi mawili juu ya Mungu kuumba ulimwengu na watu.La kwanza (1:1-2:4a) linamchora Mungu akifanya kazi kama binadamu kwa siku sita halafu kustarehe. Aliumba kila kitu kwa Neno lake (Eb 11:3; ndiye Mwanae pekee: Yoh 1:1-18). Wengine wanaona humo hata kidokezo cha kwanza cha Roho Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, katika upepo uliovuma juu ya wingi wa maji. Mungu aliona kila alichokiumba ni chema tu, lakini alipoumba mtu katika jinsia mbili akaona ni mwema sana, ni bora kuliko vingine, akamweka kuvitawala kwa niaba yake. Mwanamume na mwanamke wana hadhi sawa kwa kuwa wote wawili ni sura na mfano wake, si upande wa mwili, bali hasa kwa roho yenye uwezo wa kuelewa na kupenda kwa hiari.
Muumba anataka watu washirikiane na kusaidiana, kilele cha uhusiano wowote kati yao ni ndoa inayowafanya kuwa mwili mmoja kama Kristo na Kanisa (Ef 5:31-32).
Simulizi linalofuata (Mwa 2:2b-25) ni la zamani zaidi, nalo pia lina mafundisho makuu juu ya Mungu na mtu, hasa kwamba huyo ndiye kiumbe bora anayeweza kushirikiana na Mungu tofauti na vingine. Hali yake asili ilikuwa ya kupendeza kabisa kwa usafi wa moyo na uhai usio na mwisho, naye alitakiwa akubali kazi za Mungu na kufuata maneno yake, bila ya kujiamulia nini jema, nini baya.
[hariri] Dhambi ya asili
Mwa 3 inasimulia dhambi iliyo asili ya dhambi zote (Rom 5:12). Kwa njia hiyo tunaambiwa hali yetu mbaya haitokani na Mungu, bali na uasi wetu na wa wazee wetu (Hek 2:23-24). Pia tunafundishwa kukataa toka mwanzo vishawishi vyetu tukiamini maagizo yote ya Mungu yametolewa kwa upendo mkuu. Shetani ndiye aliyeanzisha kishawishi. Eva alipaswa asimsikilize. Kosa lake la kwanza ni kumjibu: hivyo shetani akamdanganya kwamba, eti Mungu ana kijicho, hataki watu walingane naye, ndiyo sababu aliwakataza (Yoh 8:44). Tukianza kuzingatia kishawishi tunakubali shaka juu ya wema wa Mungu kwetu katika kutuelekeza. Kwa namna hiyo walianguka watu wa kwanza waliokuwa watakatifu; kwa urahisi zaidi tutaanguka sisi wenye tabia mbaya kutokana na dhambi hiyo na nyingine nyingi.Hata baada ya dhambi Mungu anamtafuta mtu kwa upendo, ila huyo kwa aibu anamkimbia, au akijisikia analaumiwa na dhamiri, basi anatafuta visingizio hata kumlaumu Mungu kana kwamba ndiye aliyesababisha. Kwa utakatifu wake Mungu hawezi kuvumilia maovu, na kwa haki yake anataka makosa yalipwe. Ndiyo sababu tunakuta matatizo maishani, kama vile uchungu wa uzazi, kuhusiana kwa mabavu, kupata riziki kwa shida, na hasa kufa: hayo yote ni matokeo ya dhambi. Pamoja na hayo Mungu hapendi mtu yeyote apotee (2Pet 3:9), hivyo toka mwanzo aliahidi kwamba mzawa wa Eva atamponda kichwa shetani. Ndiyo habari njema ya awali kuhusu wokovu ujao.
Watu walivyoishi baada ya dhambi
Baada ya dhambi ya asili watu walianza kuzaa. Mwa 4:1-16 inatuchorea picha ya Kaini na Abeli kama wazaliwa wa kwanza waliotofautiana kiadili (1Yoh 3:11-12). Toka mwanzo mwovu na mwadilifu waliishi pamoja, wa kwanza akimdhulumu wa pili hata kumuua bila ya kujali udugu. Ikisikitishwa kufikiria mzaliwa wa kwanza kuwa muuaji wa mdogo wake, inafurahisha kwamba wa kwanza kufa alikuwa mwema, kielelezo cha Yesu aliyeuawa bila ya kosa (Eb 12:24).Toka mwanzo hao walimuabudu Mungu kwa njia ya dini, ibada na sadaka mbalimbali. Hata hivyo Mungu akakubali zile tu zilizotolewa kwa ukarimu (Eb 11:4). Tangu hapo Biblia inatuonyesha jinsi alivyopendelea wadogo kuliko wakubwa.
Kuhusu Kaini tunaonyeshwa ustawi wa dhambi ndani mwake na uongozi wa Mungu aliyemtaka ashinde dhambi bado mlangoni. Hata baada ya dhambi hiyo ambayo ni kubwa kiasi cha kumlilia Mungu alipe kisasi, yeye alizidi kumhifadhi Kaini.
Baadaye (Mwa 4:17-24) kukawa na maendeleo ya aina mbalimbali: ujenzi, ufundi, muziki, lakini hasa dhambi. Picha yake ni Lameki, mtu wa kwanza kuwa na mitara, mkatili kama nini. Ingawa hali ilikuwa ya kukatisha tamaa, kwa baraka ya Mungu watu wakazidi kuzaa na kati ya watoto wao wakapatikana waadilifu kama Henoko aliyestahili kutwaliwa na Mungu. Hata hivyo ongezeko la dhambi likasababisha maisha ya binadamu yafupike (Mwa 6:3) kwa kuwa ni kusogea mbali na Mungu, chemchemi ya uhai.
[hariri] Nuhu
Mwa 6:5-9:17 inatufundisha kwamba Mungu anachukizwa na dhambi, hivyo anataka kuondoa maovu duniani ili nchi impendeze kama alivyokusudia alipoiumba. Kwa ajili hiyo zamani za Nuhu alileta maji yafunike dunia na kuzamisha waovu. Lakini alisalimisha waadilifu katika safina kubwa ya kutosha, halafu akafunga nao agano thabiti (Eb 11:7). Hasa maji yanayokusudiwa kutakasa dunia yote ni yale ya ubatizo (1Pet 3:17-22), na safina ambayo iokoe watu ni Kanisa, ambalo ni la lazima kwa wokovu kama vile ubatizo unaotuingiza ndani yake.Uso wa nchi ulipokwishatakaswa na maji njiwa akarukaruka akachuma tawi la mzeituni unaozaa matunda ya kutengenezea mafuta. Njiwa akaonekana tena juu ya maji siku ya ubatizo wa Yesu ambapo alipakwa Roho Mtakatifu na kuyatia maji nguvu ya kutakasa watu (Mk 1:9-11; Tito 3:3-7). Maji na mafuta ndiyo mwanzo mpya kwa binadamu.
Mara alipotoka safinani Nuhu alimtolea Mungu sadaka iliyompendeza hata akaahidi hataangamiza tena binadamu kila anapostahili. Sadaka hiyo ni mfano wa ile ya Yesu msalabani, inayoadhimishwa katika ekaristi, ikituondolea adhabu nyingi na kutuletea huruma ya Mungu, yaani nafasi na neema ya kutubu (Tito 2:11-14). Hatimaye kutakuwa na hukumu (Math 24:37-41).
[hariri] Mnara wa Babeli
Mwa 11:1-9 inatufundisha kwamba kiburi na dhambi kwa jumla vinatenganisha watu wasiweze kuelewana wala kuishi pamoja. Kinyume chake katika Agano Jipya tunasikia kwamba siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, aliunganisha tena watu wa makabila mbalimbali katika kutangaza sifa zake (Mdo 2:5-12). Palipo na upendo, tofauti za lugha na utamaduni si shida.[hariri] Abrahamu (1900-1800 hivi K.K.)
Mtu huyo, aliyezaliwa Mesopotamia (Iraq) baada ya watu kubuni uandishi, ndiye mwanzo wa taifa teule la Mungu na baba wa waamini wote. Aliishi kwa kuhamahama pamoja na mifugo yake: akipitia Syria alifikia nchi ya Kanaani aliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu akashukia Misri kwa muda (Mwa 12). Lakini safari yake muhimu zaidi ni ile ya imani, kwa kuwa Abrahamu aliongozwa na Mungu siku kwa siku, katika mazuri na magumu, akisadiki ahadi zake za ajabu (Eb 11:8-19). Mchungaji huyo alikubali Mungu amchunge maisha yake yote, akamfuata bila ya wasiwasi, akituachia mfano bora wa kumshika mkono Mungu daima bila ya hofu.Hasa Mungu alimuahidia uzao mkubwa kama nyota za mbinguni, naye akaamini ingawa alikuwa hajapata hata mtoto mmoja: ndiyo imani iliyompendeza sana Mungu (Mwa 15:1-6).
Mwa 18 inamchora kama mtu mkarimu sana kwa wageni, rafiki wa Mungu anayestahili kuambiwa yote, mwenye huruma, busara na unyenyekevu katika sala. Wageni wake watatu ambao ni kama mtu mmoja tu wanadokeza Utatu Mtakatifu. Mungu alimdai Abrahamu asadiki kwamba anaweza yote kama atakavyomdai Bikira Maria (Lk 1:17), naye alidumu kumuomba awahurumie waovu kwa ajili ya waadilifu (Yak 5:16).
Mwa 19 inatuchorea uovu wa watu ambao huko Sodoma ulizidi hata kumdai Mungu alipe kisasi. Lakini kati yao mwadilifu akaokolewa, isipokuwa mke wake akaja kuadhibiwa kwa sababu aliangalia nyuma kinyume cha agizo la Bwana (Lk 17:28-33).
Mwa 21:1-21 inatusimulia jinsi Mungu alivyotimiza ahadi yake kwa kumjalia Sara amzalie Abrahamu mtoto Isaka katika uzee na utasa. Isaka ni mtoto wa imani, si wa mwili, naye ni huru, tofauti na Ishmaeli mtoto wa mtumwa ambaye hastahili kurithi pamoja na mdogo wake. Isaka, baba wa Israeli alipata baraka kuu, naye ni mfano wa watu wa Agano Jipya. Ishmaeli, baba wa Waarabu alibarikiwa pia kwa ajili ya baba yake, naye ni mfano wa Agano la Kale ambapo watu wanategemea mambo ya kimwili (kutahiriwa, kunawa, kubagua vyakula n.k.) na hivyo ni watumwa (Gal 4:21-5:1).
Mwa 22:1-19 inatuletea habari ya kusisimua kuhusu sadaka ambayo Mungu alimdai Abrahamu, yaani kumchinja Isaka. Ni kimoja kati ya vilele vya imani ya binadamu, imani inayoonyeshwa kwa matendo ya utiifu (Yak 2:21-22). Abrahamu hakusita kumrudishia Mungu kile alichopewa, akaondoka alfajiri akasafiri mpaka mahali alipoambiwa (Wayahudi wanaamini mlima huo ndipo walipojenga hekalu la Yerusalemu). Kwa niaba ya waamini wote Abrahamu alikuwa tayari kumchinjia Mungu mwanae pekee ampendaye. Lakini atakayemtoa kweli Mwana pekee ni Mungu Baba (Yoh 3:16). Mwanae ndiye mwanakondoo aliyeuliziwa na Isaka na ambaye Mungu akajipatia juu ya mlima Kalivari alioupanda huku amejitwika sio kuni bali mti wa msalaba. Abrahamu aliamini uwezo wa Mungu juu ya mauti na hasa uaminifu wake kwa ahadi alizompa: kwa hiyo akarudishiwa mwana hai kama mfano wa ufufuko, na katika yeye, yaani katika mzawa wake, watu wote wakabarikiwa. Maisha ya imani yanadai daima sadaka, hasa ya mambo yanayopendwa zaidi (Rom 12:1-2): ndiyo njia ya kujaliwa baraka zinazopita ubinadamu wetu.
Mwa 24 inasimulia kirefu jinsi Abrahamu kabla hajafa alivyomfanyia mpango wa ndoa Isaka kufuatana na mila zao, ila alikataza kabisa asirudi kwao, bali kwa vyovyote abaki katika nchi ile aliyoahidiwa na Mungu. Hivyo imani izidi kuongoza uzao wake kama ilivyomuongoza mwenyewe.
[hariri] Watoto wa Isaka: Esau na Yakobo
Kadiri ya Mwa 25:19-34, Rebeka alimzalia Isaka watoto pacha wenye sura na silika tofauti, Esau na Yakobo. Wa kwanza analaumiwa hasa kwa kupuuzia baraka ya Mungu iliyokuwa haki ya kifunguamimba: kwa sahani ya dengu alikubali kukosa neema zile zote alizojitwalia Yakobo kwa imani yake (Eb 12:16-17).Mwa 27 inasimulia jinsi Yakobo, akifundishwa na mama yake, alivyoweza kubarikiwa na baba. Ingawa uongo wake haukubaliki (Hos 12:3-5), Mungu alithibitisha baraka ya Isaka kadiri ya desturi yake ya kumpendelea mdogo: hivyo Yakobo, aliyekimbia nchi yake ana fimbo tu, alirudi miaka ishirini baadaye ana wake 4, watoto 11 na mifugo wengi ajabu (Mwa 32). Kabla hajaingia nchi yake Mungu alishindana naye usiku kucha akalazimika kumbariki na kumtajia jina jipya, Israeli.
[hariri] Yosefu na ndugu zake kushukia Misri (1700 hivi K.K.)
Kama kawaida ya mitara, kulikuwa na upendeleo na wivu. Hasa Yosefu alichukiwa na kaka zake wote, ingawa alikuwa mnyofu hata kuwasimulia ndoto zake za ajabu (Mwa 37:2-11). Kijicho na chuki vilifikia hatua ya kuwafanya watamani kumuua. Walipopata nafasi walifanya njama, ingawa si wote. Mwisho uamuzi ukawa kumuacha hai lakini kumuuza kama mtumwa kwa wafanyabiashara walioelekea Misri (Mwa 37:12-36). Lakini katika maovu ya binadamu Mungu akazidi kushughulikia taifa lake teule. Hivyo Yosefu akawa mfano wa Yesu ambaye alichukiwa bure tu akauawa msalabani kwa wokovu wa wadogo zake wakosefu.Mwa 39 inaonyesha jinsi Yosefu alivyozidi kumtiii Mungu na kukwepa dhambi. Hivyo baada ya majaribu mbalimbali akatukuzwa kuwa liwali wa Farao kwa nchi yote, hasa kwa usimamizi wa akiba ya chakula (Mwa 41:1-49) kwa ajili ya miaka saba ya njaa aliyotabiri. Kadiri ya mpango wa Mungu njaa hiyo ikawalazimisha kaka zake waje kumuinamia, naye hakulipa kisasi; halafu, kama vile alivyotafsiri ndoto mbalimbali, aliwafafanulia maana ya matukio ya maisha yao katika mpango wa Mungu: kwamba ndiye aliyemtuma Misri kusudi awaokoe (Mwa 45:1-15).
Mwa 46:1-7 inasimulia Yakobo na wazawa wake wote, jumla wanaume 70, walivyohamia Misri. Lakini hawakusahau nchi waliyoahidiwa na Mungu: ndiyo sababu Yakobo na Yosefu walidai waapiwe kuwa watakuja kuzikwa kwao (Mwa 49:29-50:26). Kabla ya kufa Yakobo aliwabariki watoto wake 12 na kwa namna ya pekee Yuda ambaye atatawala moja kwa moja (Mwa 49:8-12).
[hariri] Utumwa wa Misri na wito wa Musa (1250 hivi K.K.)
Wanaisraeli waliishi Misri kama wageni tu zaidi ya miaka mia nne (Mdo 7:6-16) wakiongezeka kiasi cha kuwatisha wenyeji wao: ndiyo sababu wakaanza kudhulumiwa mwaka 1300 hivi K.K.Hasa katika kuwakomboa utumwani, Mungu alijionyesha mtetezi wa haki za maskini. Pamoja na kushurutishwa kufanya kazi wasioipenda, ilitolewa amri ya kuua watoto wao wote wa kiume: lakini mpango huo haukutekelezwa sawasawa (Kut 1:7-22).
Mmoja kati ya watoto waliookolewa katika hatari hiyo ni Musa, wa kabila la Lawi (Kut 2:1-10; Eb 11:23; Mdo 7:17-22). Kisha kukimbia Misri Musa akaoa Mmidiani (Kut 2:11-22; Eb 11:24-27; Mdo 7:23-29): alipokuwa anachunga mifugo ya mkwewe kwenye mlima Sinai akaitwa na Mungu kutoka ndani ya kichaka kinachowaka moto kisiteketee. Mungu alimchagua ingawa ana kigugumizi yaani anaonekana hafai kushindana na Farao. Mungu akasisitiza aende mwenyewe, naye atatumia uwezo wake wa Kimungu kumlazimisha Farao. Kadiri Musa alivyoomba, Mungu alimfunulia jina lake takatifu YHWH ambalo linaeleweka kiasi tu, kama vile fumbo la Mungu mwenyewe (Kut 2:23-3:20; Mdo 7:30-35).
[hariri] Mapigo ya Wamisri
Mungu alipomtuma Musa kwa Farao alijua tayari huyo atakataa kuwaruhusu Waisraeli waende zao, mpaka aone mapigo yake kwa Wamisri. Kwa kuwa ulihitajika muda kuleta ukombozi, iliwabidi Waisraeli wawe na imani na subira hadi ahadi za Mungu zitimie. Lakini binadamu hatupendi kungojea ukombozi: hivyo Waisraeli wakaanza kunung’unika (Kut 5:1-6:1). Hata hivyo Mungu akaendelea na mpango wake.Maajabu aliyoyatenda huwa yanatokea Misri lakini si yote kwa wakati mmoja wala si kwa kiasi kile alichosababisha Musa kwa fimbo yake (Kut 6:28-7:7). Tuna orodha mbalimbali za mapigo hayo, lakini kwa kawaida yanahesabiwa kumi: maji ya mto Naili kuwa mekundu kama damu, vyura kujaa nchi, chawa, nzi, tauni, majipu, mvua ya mawe, nzige, giza na hatimaye kifo cha wazaliwa wa kwanza wa kiume wa watu na wa wanyama. Adhabu hizo ziliwapata Wamisri, lakini si Waisraeli: hivyo ilikuwa wazi kuwa Mungu anabagua watu wake na watu waovu.
Katika pigo la kumi Waisraeli waliopolewa kwa kuipaka milango yao damu ya mwanakondoo (Kut 11:1-10; Mdo 7:36-37; Eb 11:28). Hivyo Mungu aliwaandaa watu kupokea imani kwa Yesu Kristo, Mwanakondoo wa kweli na Mkombozi wa waliokuwa watumwa wa dhambi, shetani na kifo (Yoh 19:36; 1Kor 5:7; 1Pet 1:18-20). Hiyo ni wazi katika ibada iliyoagizwa ifanyike kila mwaka (Kut 12:1-14), yaani Waisraeli wale nyama ya mwanakondoo dume asiye na hila, pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga ya majani machungu. Yesu akaifanya ibada hiyo iwe ibada kuu ya agano jipya la milele, akiagiza tuifanye kwa ukumbusho wake, si tena kwa ukumbusho wa kutoka Misri (1Kor 11:23-26).
[hariri] Safari ya kuendea Nchi ya ahadi
Kut 12:29-42 inasimulia Waisraeli wote walivyokimbia Misri pamoja na mifugo yao waliposikia mayowe kutoka nyumba za majirani wao wote. Katika safari yao wakaongozwa na Mungu kwa sura ya wingu mchana na ya moto usiku (Kut 13:17-22; Yoh 8:12): hivyo Mungu alionyesha wazi kuwa hawaachi hata kidogo bali anawashughulikia kwa namna tofauti kadiri ya mahitaji.Kut 14:5-31 inasimulia jinsi Wamisri, kisha kuwalilia wafu wao, walivyoanza kuwatafuta Waisraeli kwa farasi na magari wakawakuta karibu na bahari ya Shamu. Lakini Waisraeli walivuka bahari kama kwamba ni nchi kavu, kwa kuwa maji yamegawanyika. Kumbe Wamisri wakazama kwa kuwa maji yamerudi mahali pake (Eb 11:29). Asubuhi Waisraeli wakaona maiti za Wamisri wote zikielea wakamshangilia Mungu aliyewaokoa (Kut 15:1-21 inatuletea wimbo ambao maneno yake ni kati ya yale ya kale zaidi katika Biblia). Hivyo Mungu aliwaokoa tena watu wake katika maji, na huu pia ni mfano wa ubatizo ambao unaadhimishwa hasa usiku wa Pasaka. Hata katika hatari ya kukandamizwa Mungu alidai Waisraeli watulie kwa imani ya kuwa ushindi ni wake tu. Tena walitakiwa wasiyasahau kamwe mang’amuzi hayo, kwa kuwa ndiyo msingi wa imani ya dini yao. Sisi vilevile tunatakiwa kukumbuka daima ubatizo wetu ambapo Mungu ametuokoa.
Baada ya ushindi wa Pasaka safari ikaendelea mpaka kufikia nchi aliyoahidi Mungu, ila Waisraeli wakaja kusahau uweza wake na kumlalamikia kipumbavu hata kumchosha. 1Kor 10:1-11 inatuonya tusifanye vile. Kama kawaida malalamiko ya kwanza yalihusu kula na kunywa (Kut 15:22-17:7). Mungu aliwakubalia kwa kuwateremshia kwale halafu mana: hasa chakula hicho kiliwashangaza Waisraeli wakazidi kukikumbuka hata wakamdai Yesu awapatie tena kama kweli ndiye Musa mpya. Yesu akawajibu kuwa mwenyewe ndiye chakula cha uzima kutoka mbinguni kinachotulisha safarini hapa (Yoh 6:22-59). Vilevile kuhusu maji, Mungu aliyatokeza katika mwamba huko Masa au Meriba, lakini alichukizwa sana na matendo yao (Eb 3:15-19).
Shida nyingine ya kawaida kwa makabila ya wahamaji ni kupigana vita. Waisraeli walilazimika kufanya hivyo na Waamaleki, wakapata ushindi si kwa nguvu zao, ila kutokana na sala ya Musa, mwombezi wao (Kut 17:8-16). Sisi taifa la Mungu tunatakiwa tutegemee sala kuliko uhodari wetu, na daima tuwe na watu wenye kumuinulia Mungu mikono yao kama Musa jangwani.
Agano la Mlima Sinai
Walipofikia mlima huo wa kutisha, Mungu alimuita Musa aupande ili aseme naye, huku wengine wakibaki chini. Hapo akampa Musa masharti ya agano lake na Waisraeli (Kut 19). Akiwa Muumba na hasa Mkombozi wao alidai waishi kitakatifu kwa kushika amri kumi, ambazo tatu zinahusu heshima kwake na saba uhusiano na watu wengine (Kut 20:2-17). Ndiyo mawe mawili ambayo Musa alipewa halafu Yesu akayakamilisha katika amri kuu ya upendo kwa Mungu na kwa jirani (Mk 12:28-34). Amri hizo zinaweza kujulikana na kukubaliwa na mtu yeyote mwenye mapenzi mema, lakini Mungu alipenda kutusaidia tujue kwa urahisi na hakika zaidi tufanye nini ili kumpendeza, tuwe watu wake naye awe Mungu wetu kwelikweli. Agano hilo upande wa Mungu ni imara kwa kuwa yeye ni mwaminifu kabisa, shida iko upande wetu tulio geugeu, tukiahidi tusitekeleze. Ndiyo sababu likahitajika agano lingine lililofungishwa na Yesu Kristo (2Tim 2:11-13).[hariri] Ndama ya dhahabu
Kut 32 inasimulia uasi wa Waisraeli ulivyofikia kilele chake walipojitengenezea mungu wa dhahabu mwenye sura ya fahali (Biblia kwa dharau inasema “ndama” na “mla nyasi”). Hata Haruni, kaka yake Musa, alikubali kufuata matakwa yao huku mdogo wake akichelewa mlimani (Mdo 7:38-42). Musa akambembeleza Mungu asiwaangamize watu wake, hivyo akawa mfano bora wa mwombezi, kwa kuwa hakujali ahadi ya Mungu ya kumfanya chanzo cha taifa lingine kubwa. Kazi hiyo ni hasa ya Bwana Yesu ambaye aliwatetea watu wake kwa kumwaga damu yake, na anazidi kuwaombea kwa Baba yake (Eb 7:25-27).[hariri] Mungu kujifunua tena kwa Musa
Kut 33:18-34:9 inasimulia jinsi Mungu alivyokubali kiasi ombi la Musa la kumuonyesha utukufu wake; badala ya kumuonyesha uso wake (Yoh 1:18) alijifunua kwake kwa kulitangaza na kulifafanua jina lake: YHWH ni mwingi wa rehema na uaminifu, anawaonea wivu watu wake, yaani hawezi kukubali waabudu miungu mingine kwa hasara yao. Ndiyo sababu alipoagana nao kwa kuandika tena amri zake kumi katika mawe, pamoja na kuahidi kuwafukuza wenyeji wa nchi takatifu ili kuwapatia nafasi Waisraeli, aliwaagiza wasichanganyikane nao wasije wakavutwa katika Upagani. Hasa alikataza ndoa za mseto ili kulinda usafi wa imani. Kwa namna ya pekee Kristo analipenda na kulionea wivu Kanisa lake analolitaka bikira safi katika imani na maadili (2Kor 11:2; Ef 5:25-27): hivyo tunaposhirikiana na watu wengine tuwe macho tusifuate mawazo, maneno na matendo yao, bali tushuhudie imani na upendo kwa maisha yetu tofauti na ya kwao (Yoh 17:15-17).[hariri] Mambo ya Walawi
Kitabu hicho cha tatu kimejaa hasa sheria za ibada zenye kulenga utakatifu wa makuhani na wa sadaka. Watu wa kabila la Lawi tu ndio walioruhusiwa kushughulikia ibada, tena kati yao ukoo wa Haruni tu ndio makuhani kamili. Kutokana na kazi hiyo Walawi hawakupewa sehemu ya nchi takatifu, ila Mungu mwenyewe ndiye fungu lao. Lakini taifa lote lilitakiwa liwe takatifu kutokana na uhusiano wake na Mungu (Law 19:1). Polepole maana ya utakatifu huo ilizidi kueleweka si kukwepa unajisi wa kiibada tu, bali unategemea hasa mwenendo mwadilifu.[hariri] Hesabu
Kitabu cha nne kinaitwa hivyo kwa sababu kinaleta hesabu mbalimbali, hasa ya idadi ya Waisraeli: wanaume wa kuweza kwenda vitani walikuwa 603,500 (mbali na Walawi waliohesabiwa peke yao: wanaume 22,000 wakiwa pamoja na watoto wa kiume); ukiongeza wanawake na watoto mpaka umri wa miaka ishirini, basi jumla yao iliweza kufikia watu milioni tatu, ingawa si lazima kuamini idadi hiyo ni sahihi (pengine namba hizo hazilingani katika makala kwa kuwa ilikuwa rahisi kukosea wakati wa kunakili).Uzito wa kazi ya kuwaongoza watu wengi hivyo wanaonung’unika kila mara ulimchosha Musa hata akamuomba Mungu tena ampunguzie mzigo au amuue kabisa (Hes 11:1-30). Musa alieleza shida yake kama rafiki kwa mwenzake, kwa unyofu uleule wa watu wengine wa Mungu katika Biblia. Mungu akamkubalia akawashirikisha watu sabini roho yake kwa ajili ya uongozi katika ngazi mbalimbali. Huo pia ni mfano wa Agano Jipya, ambapo askofu hawezi kuchunga waamini peke yake, bali anahitaji msaada wa viongozi wa daraja za chini, yaani mapadri na mashemasi (Mdo 6:1-6). Katika nafasi hiyo Musa alimueleza Yoshua kwamba hawaonei kijicho kwa kupewa karama, tena angependa kama Waisraeli wote wangekuwa manabii. Hamu hiyo ikatimia siku ya Pentekoste: katika Kanisa wote wanapewa Roho Mtakatifu na kuwa manabii, hata wanawake na watoto (Mdo 2:16-18).
Kinyume chake Hes 12 inasimulia kijicho kilivyowafanya dada na kaka wa Musa wamseme wakijidai nao pia ni manabii. Lakini Mungu akawaeleza kuna namna mbalimbali za unabii, na Musa ni wa pekee. Kisha akatoa adhabu ambayo ikaondolewa kwa maombezi ya Musa tu: ndiyo sababu anasifiwa kwa upole wake. Kijicho kitasumbua daima taifa la Mungu, hata katika Agano Jipya (1Kor 12:1-31; 14:37-38).
Waisraeli walipofikia mipakani mwa nchi takatifu walituma wapelelezi ili waivamie, nao waliporudi walisimulia uzuri wake, lakini pia walitisha kwa kuzidisha habari za wananchi na miji yao (Hes 13). Hapo Waisraeli wakaanza kunung’unika usiku kucha (Hes 14) wakapanga kuwaua kwa mawe Kalebu na Yoshua waliotaka kuivamia nchi bila ya hofu kwa jina la Bwana. Lakini Mungu akaonyesha utukufu wake na kutisha ataleta tauni ili kuwaangamiza wote kwa ukaidi wao. Kwa maombezi ya Musa, akakubali kuwahurumia lakini akaamua warudi jangwani na kuzungukazunguka huko mpaka wafe wote; ila watoto wao pamoja na Kalebu na Yoshua ndio watakaoingia nchi takatifu kuimiliki. Maana ya kiroho ni kwamba hatutakiwi kuzitia shaka ahadi za Mungu; hata zikionekana ngumu kupatikana, ni lazima tuwe na moyo mkuu na imani hata tukabili vipingamizi vyovyote.
Kinyume chake, Waisraeli walipoamua kuivamia nchi kwa kusikitikia adhabu waliyopewa wakashindwa kabisa, maana ni lazima tumtii Mungu kwa wakati wake. Pia kughairi kutokana na matatizo kunaweza kukatusukuma tutende namna ambayo haimpendezi tena; ni lazima tuchukue majukumu ya matendo yetu na kukubali adhabu au matatizo tuliyojitakia:majuto hayo yanafaa kwa kuonyesha utiifu kwa Mungu (Zab 119:71).
Manung’uniko ya Waisraeli katika safari yao jangwani yakawaletea adhabu nyingine, mojawapo ile ya kugongwa na nyoka wengi wenye sumu kali. Lakini walipoomba msamaha, Mungu akamuagiza Musa atengeneze nyoka wa shaba na kumuinua juu ya mti ili mtu aliyeumwa akimtazama tu apate kupona (Hes 21:4-9). Ufafanuzi wa tukio hilo ulitolewa na Yesu mwenyewe: ndiye aliyeinuliwa juu ya mti wa msalaba ili watakaomtazama kwa imani wapate kuishi (Yoh 3:14-15).
Kumbukumbu la Torati (Sheria)
Kitabu hicho cha mwisho cha Torati kiliandikwa kama miaka 600 baada ya Musa, ingawa kina namna ya hotuba tano alizoweza kuwatolea Waisraeli kabla hajafa. Kinapitia upya matukio ya wokovu ya wakati wa Musa kikifaidika na ujumbe wa manabii, hasa Hosea. Kwa msingi huo, kitabu hiki kinasisitiza sana upendo kwa Mungu, uaminifu kwa agano la mlima Sinai pamoja na tuzo na adhabu zitakazotolewa kufuatana na matendo ya Waisraeli. Katika maneno yake yote ya kitabu hiki, maarufu ni hasa yale ya 6:4-9 ambayo Mwisraeli yeyote anayakariri kila siku katika sala na kuyashika pengine neno kwa neno.Maneno mengine muhimu sana yapo 26:5-10: ni kama kanuni ya imani ambayo Mwisraeli alikuwa anaiungama mbele ya Mungu wakati wa kumtolea malimbuko ya ardhi. Hivyo alikuwa akikiri amepewa yote na Bwana, halafu akaweza kuyafurahia mavuno.
Baada ya hotuba hizo, Kumb 31:1-8 inasimulia jinsi Musa alivyomuachia Yoshua uongozi wa Waisraeli wote kwa kumwekea mikono (Hes 27:12-23). Musa alifikia mpakani mwa nchi takatifu asikubaliwe kuiingia kama adhabu ya makosa yake, ila alionyeshwa yote kutoka mlimani (Kumb 32:48-52) halafu akafariki (Kumb 34). Kazi aliyopangiwa iliishia huko, mwingine akampokea na kuendeleza ukombozi wa Kimungu. Binadamu wote ni vyombo tu vinavyotumika kwa muda fulani, halafu vinaweza kuachwa. Kumbe Mungu ndiye mtendaji mwenyewe ambaye hasinzii wala halali, bali anazidi kuwashughulikia watu wake. Kwa imani hiyo tuwe daima tayari kuwaachia wengine nafasi yetu.
[hariri]
Vitabu vinavyofuata katika Biblia ya Kiebrania (Yoshua, Waamuzi, Samweli na Wafalme) vinataka kuthibitisha kwamba kweli ikawa kama hiki kinavyosema: Waisraeli walipofuata agano (wakati wa Yoshua) waliteka nchi ya ahadi na kuifurahia, lakini walipozidi kuasi (wakati wa Waamuzi, Samweli na Wafalme) walikuja kunyang’anywa nchi ile yote, kwanza sehemu nzuri zaidi (kaskazini), halafu ile hafifu zaidi (kusini). Hapo Waisraeli wote wakajikuta tena utumwani katika nchi ya kigeni kama kabla ya Musa, wakikosa hata [[sanduku la agano], lililopotea wakati wa maangamizi ya Yerusalemu na hekalu lake, baada ya wao kufikia hatua ya kula watoto wao kutokana na njaa.Vitabu hivyo vilikamilishwa wakati wa kukaa uhamishoni Babeli, vikiwa jibu la swali kuu lililowakwaza huko: je, Mungu wetu ameshindwa? Waandishi walichagua matukio mbalimbali ya historia baada ya Yoshua ili kuthibitisha kuwa aliyeshindwa ni Israeli, si Mungu. Historia hiyo inaonyesha mfululizo wa maasi hata baada ya Mungu kutuma waamuzi na manabii wake ili kuwaonya Waisraeli na kuwaelekeza upya.
Lengo la waandishi halikuwa kutunza kumbukumbu za mambo yote kwa usahihi na ukamilifu, bali kuelekeza njia ya kupata wokovu hata baada ya Israeli kuonekana imekoma moja kwa moja. Kama vile Biblia nzima, vitabu hivyo vinalenga wokovu wetu, vikihakikisha kuwa Mungu anaweza kuleta mwanzo mpya hata hali ikiwa mbaya namna gani. Ndiyo sababu habari ya mwisho kabisa ni ya kuleta tumaini: kwamba mfalme Yekonia alitolewa gerezani (alipokaa miaka 37) na kufanywa mgeni wa kudumu mezani pa mfalme wa Babeli.
[hariri] Yoshua (1210-1200 hivi K.K.)
Kitabu cha sita cha Biblia kinatupasha habari za uvamizi wa nchi takatifu ambao Waisraeli waliufanya chini ya Yoshua, ambaye ni mfano wa Yesu (hata jina lao kwa Kiyahudi ni moja, linalotafsiriwa “Mungu anaokoa”): ndiye aliyewaingiza watu katika nchi ya ahadi, si Musa.Mara baada ya kushika uongozi, Yoshua alituma wapelelezi nchini; huko Yeriko, mji wa zamani kuliko yote ya dunia, walisaidiwa na Rahabu, kahaba aliyeamini kuwa ushindi utakuwa wa Mungu wa Israeli (Yos 2): kwa hiyo akaokolewa pamoja na ndugu zake, tena akajaliwa kuwa bibi wa babu wa mfalme Daudi, hata akatajwa na Injili kama bibi wa Yesu Kristo (Math 1:5-6), halafu akachukuliwa kama mfano wa imani (Eb 11:31) na wa matendo mema (Yak 2:25).
Yoshua aliwavusha Waisraeli pakavu kati ya mto Yordani (Yos 3-4) na hivyo akawaingiza katika nchi takatifu. Hapo ikawabidi kwanza wafunge tena agano na Mungu kwa kutahiriwa wanaume wote na kwa kuadhimisha Pasaka ambapo kwa mara ya kwanza walikula mazao ya nchi hiyo waliyoahidiwa: ndio mwisho wa mana na wa kipindi cha jangwani (Yos 5:1-12). Hata sisi tutaacha kula mkate toka mbinguni tutakapoingia pale tulipoahidiwa.
Baada ya matendo hayo ya kidini Mungu alimtokea Yoshua kama amirijeshi wa Israeli ili kumhakikishia kwamba mwenyewe ataongoza mambo, hivyo Yoshua amtegemee akijisikia chombo chake tu (Yos 5:13-15). Ni rahisi kwa kila binadamu aliyeshika uongozi kujisikia mwenyewe na hivyo kuacha kumtegemea Mungu. Kumbe Yoshua kwa kupokea ujumbe huo akaweza kushinda watu wenye maboma, nguvu na silaha kali kuliko Waisraeli. Kwamba hiyo ni nguvu ya Mungu inaonekana wazi hasa katika simulizi la kuteka Yeriko (Yos 6:1-21): huko Waisraeli walifanya maandamano ya ibada mpaka kuta za mji zikaanguka. Vita vyetu vya kiroho na vya kitume vitegemee hasa sala. Baada ya vita vingi Yoshua akayagawia makabila 12 ya Israeli nchi yote, ikiwa ni pamoja na sehemu zilizobaki chini ya wenyeji (Yos 12:1-13:14). Huko Shekemu aliwadai wote wachague kumtumikia YHWH au miungu mingine, akisisitiza ugumu wa kumtumikia sawasawa Mungu aliye mtakatifu na mwenye wivu kwa watu wake. Lakini wao walikubali kwa moyo wote kumtumikia Mungu tu, wakasimamisha jiwe kubwa kama kumbukumbu (Yos 24:1-28).
Kabla hajafa Yoshua akawaita Waisraeli wote ili kuwaimarisha katika imani na umoja kwa kuwakumbusha maajabu waliyotendewa na Mungu na kwa kuwahimiza wamuonyeshe shukrani (Yos 23). Kukumbuka ni jambo muhimu ili tuishi kwa imani bila ya kudanganywa na maisha yanayosahaulisha kwa urahisi mambo ya Kimungu.
by Meshack Ezekia Kitova
No comments:
Post a Comment