Labels

Tuesday, October 2, 2012

KWA NINI MUNGU ANATAKA TUENENDE KWA ROHO?


 Ukisoma katika warumi 8:14 Biblia inasema “kwa kuwa wote wanaoongozwa  na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” na pia Paulo kwa wagalatia anasema” Basi nasema Enendeni kwa Roho,wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili Wagalatia  5:16. 
Hapa tunaona jinsi Paulo anavyosisitiza kwa makanisa ya Rumi na korinto kuhusu suala zima la kuongozwa  na Roho  Mtakatifu. Anawaambia warumi kwa  kuwa wote wanaongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana  wa Mungu maana yake haijalishi  ana umri gani, ni wa dhehebu gani, jinsia gani maadamu anaongozwa  na Roho wa Mungu huyo ni mwana wa Mungu na bado anawaagiza wagalatia akisema Basi nasema  enendeni   kwa Roho………….. anaposema enendeni maana  yake  mkiongozwa  na Roho, au mkimfuata  Roho katika yale anayowaagiza. Maneno haya yanaonyesha  zipo sababu za msingi  kwa nini tunatakiwa kuongozwa  na Roho  sasa hapa sizungumzii kazi za Roho mtakatifu najua zipo kazi nyingi anazozifanya Roho Mtakatifu lakini mimi nazumgumzia sababu za kuongozwa  na Roho Mtakatifu, ambaye ndio agano jipya la Mungu kwetu (Yeremia 31:31) katika hiyo Yeremia Neno linasema “Angalia siku zinakuja asema Bwana nitakapofanya  agano jipya na nyumba ya Israel. Sasa ukiendelea kusoma mistari inayofuata utaona anazungumzia habari za kutia sheria yake katika mioyo ya watu.
Sasa hili ndilo agano jipya la Mungu pamoja na wanadamu. Sasa usipojua kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho na siyo akili zako, au mazoea, au taratibu za kwako n.k. hautajua umuhimu wa kuongozwa na Roho Mtakatifu na pili hautaona sababu za kuongoza na Roho Mtakatifu. Sasa  lengo la ujumbe huu ni kukufundisha sababu za msingi  za kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho Mtakatifu na siyo akili  zako au mawazo yako. Sasa baada ya utangulizi huo mfupi na tuangalie sababu hizo za msingi. 

Moja,
Ili tusizitimize tamaa za mwili wagalatia 5:16
“Basi nasema enendeni kwa Roho , wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Tunatakiwa tuenende kwa Roho ili tusizitimize tamaa za mwili. Siku zote mwili na Roho ni maadui nia ya mwili ni mauti na nia ya Roho ni uzima na amani (Warumi  8:7). Maana  yake siku zote mwili utakuongoza kufanya mambo ambayo mwisho wake ni mauti ya kiroho na  hata kimwili pia.
Utakuongoza katika  tamaa zake, sasa usipoongozwa na Roho huwezi  kujizuia kutekeleza tamaa za mwili na kwa sababu hiyo wewe si mwana wa Mungu   na mtu wa namna  hii hataingia mbinguni kamwe.  Katika 1Wakorinto 6:9-10 anasema “Au  hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme  wa Mungu? Msidanyanyike, waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala  waabudu  sanamu, wala wazinzi, wala  wafiraji, wala walawiti, wala walevi, wala watamanio, wala walevi wala   watukanaji, wala wanyang’anyi.Sasa utakapoongozwa na Roho Mtakatifu utaratibu wake utakuacha huru mbali  na hayo mambo ya mwili au nia ya mwili na utakuongoza katika uzima  na amani  na kulitenda tunda la Roho ambalo  ni upendo, furaha, amani, uvumilivu utu wema  , fadhii, uaminifu, upole na kiasi “Wagalatia 5:22-23”.
 Mbili,
Ili tupate kuyaelewa mafumbo ya Mungu  na kuyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni.
1Wakorinto 2:10 inasema “ Lakini  Mungu  ametufunulia  sisi kwa Roho, maana Roho huchunguza yote hasa mafumbo ya Mungu” na ule mstari wa 13 unasema “ Nayo twayanena , si kwa maneno yanayofundishwa  kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa  na Roho, tukiyafasiri mambo ya Rohoni  kwa maneno  ya Rohoni. Hapa najua walio  wachungaji, walimu  wa neno la Mungu au viongozi wa vikundi mbalimbali vya kiroho watanielewa zaidi.
sikiliza Roho Mtakatifu ndiye mwenye uwezo wa kuchunguza kilichopo kwenye ufahamu wa Mungu kuhusu wewe, ndoa yako, kanisa lako, biashara yako, masomo yako, nchi  yako n.k. sasa akishachunguza ndiyo anakujulisha maana wewe ulikuwa hujui. Pia Roho Mtakatifu ndiye  anayekusaidia kuyanena, kuyafundisha au kuyafafanua maneno ya Mungu kwa  watu wake,  anaposema kuyafasiri  maana yake kuyafundisha mambo ya Rohoni kwa jinsi / namna ya Rohoni.
 Hivyo kama  wewe ni kiongozi au mwalimu wa neno  la  Mungu, ukiongozwa na Roho, yeye atakuongoza / atakusaidia kuwafundisha hao watu neno la Mungu kwa jinsi  ya Rohoni yaani kwa mfumo wa Rohoni kulingana na watu ulio nao, maana yeye ndio mtunzi wa hilo Neno,soma mwenyewe 2Petro 2:21” maana  unabii haukuletwa popote kwa mapenzi  ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
Tatu,

Ili   tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu na kuyapokea mambo ya Roho na Mungu .
Iwakorinto 2:12 inasema “Lakini sisi hatukupokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa  na Mungu” na ule wa 14 unasema “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei  mambo ya Roho wa Mungu maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya Rohoni. Unapoongozwa  na Roho Mtakatifu ndipo anapokusaidia kujijua wewe mwenyewe vizuri. Anaposema  upate kuyajua yale ambayo Mungu amekupa katika maisha yako.Roho mtakatifu atakusaidia kujua aina ya vipawa  ulivyonavyo, karama za Rohoni ulizonazo, huduma ulizonazo kama umeitwa huko, atakusaidia kujua vizuri unaweza kufanya  nini na nini  huwezi, kipi ufanye  na kipi usifanye, atakusaidia kujua baraka zako za kiroho  na kimwili pia. Kwa kifupi  atakusidia kulijua kusudi   la Mungu katika maisha yako na vipi ufanye ili uweze kulifikia hilo kusudi na zaidi  atakupa upako/ nguvu za kuweza kuyapokea yale yote anayo kuagiza ili uweze kulifikia kusudi lake kwako na kuzirithi baraka zako maana katika zaburi 32:8  anasema “Nitakufundisha  na kukuonyesha njia utakayoienda nitakushauri, Jicho langu likikutazama”.
 Nne,
Ili atusidie kuomba yale tunayotakiwa kuyaomba kwa wakati huo.
Warumi 8:26” kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua   kusikoweza kutamkwa”. Udhaifu unaozumgumziwa ni wa namna  mbili moja si rahisi kwa jinsi  ya  mwili kuomba kwa muda mrefu kwa sababu mwili ni dhaifu na pili udhaifu tulionao ni kushindwa kuomba jinsi inavyotupasa kuomba.
 Sasa  tunapoongozwa na Roho, maana yake moja anatusidia tuweze kuomba na zaidi anatufundisha namna ya kuomba  na kutuongoza  yapi tuyaombee kwa wakati huo  au kipindi hicho. Mfano wewe unaweza ukawa unaomba upako wa Roho Mtakatifu katika huduma na yeye  Roho Mtakatifu, anajua kwamba  ameshakutia mafuta  na shida uliyonayo ni kutokujua namna ya kushirikiana na upako wake ulio juu yako. Hivyo yeye atakuongoza kuomba kwa habari ya kushirikiana  na upako aliouweka juu yako. Kwa  kifupi yeye kwa sababu ndiye mwenye maisha yako atakuongoza siku zote kuomba yale unayotakiwa kuyaomba kwa majira hayo iwe kuhusu masomo, ndoa, kanisa, nchi n.k.
Tano,
Ili atuongoze katika kufanya maamuzi.
 2Wakorinto 3:17  Basi Bwana ndiye Roho, walakini alipo Roho  wa Bwana, hapo ndipo penye  uhuru”  pia ukisoma warumi 8:1-2 inasema  “sasa, basi hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu, kwa sababu sheria ya Roho wa uzima  ule ulio katika kristo Yesu imeniacha huru, mbali  na sheria ya dhambi na mauti”  kufanya maamuzi ni sehemu  ya maisha ya mwanadamu. Yapo  maamuzi  mengi sana  ambayo mwanadamu anatakiwa kufanya na hawezi kukwepa kuyafanya.
Sasa Mungu kwa kulijua  hilo ametupatia Roho Mtakatifu ili atusaidie katika kufanya  maamuzi. Roho Mtakatifu anapokuwa Bwana   kwako, yaani  mtawala, kiongozi ndipo anapokupa uhuru juu ya kufanya maamuzi katika maisha yako. Maana yake ulikuwa hujui nifanye nini? Niamueje ? Sasa yeye anakuletea uhuru ndani wa  kufanya jambo ambalo anajua ni la mafaniko  kwako. Kumbuka siku zote nia ya Roho ni uzima na amani.
 Huenda ziko sababu nyingi ni kwa nini unatakiwa uenende  kwa Roho, lakini hizi tano ndizo Mungu alizonipa tuweze kushirikiana kujifunza. Ni imani yangu kwamba utakapoamua kutaka na kupenda kuongozwa na Roho ndipo utakapoona Mungu akijifunua kwako .

No comments: