Ukifuatilia
historia ya kilema huyu aliyeponywa utaona ya kuwa alikuwa hivyo tangu
kuzaliwa, na alipopona alikuwa na umri uliopita miaka arobaini (Matendo
ya Mitume 4:22).
Siri
ya muujiza huu ilikuwa ni nini? Je! kilema huyu alipona kwa uweza wa
Petro na Yohana au kwa uweza wa jina la Yesu Kristo?
Nauliza
maswali haya kwa kuwa watu wengi wakimwona mtu anatumiwa na Mungu katika
uponyaji wanaweka imani katika mtu huyo badala ya kuweka imani katika
jina la Yesu Kristo.
Na
ndivyo ilivyokuwa wakati kilema huyu alipopona, watu waliokuwa hekaluni
waliwashangaa wakina Petro na Yohana kama vile kilema huyo alipona kwa
uwezo wao. Petro alipoona hali hiyo, aliamua kuwaeleza watu hao ukweli
ulivyo; alisema hivi;
“Basi
(Yule aliyekuwa kilema) alipokuwa akiwashika Petro na Yohana, watu wote
wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani,
wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi
Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kama
kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi au kwa utauwa (utakatifu)
wetu sisi?”
(Matendo ya Mitume 3:11 – 12).
Petro
alikuwa anafanya jambo muhimu hapa kwa kusaidia kubadilisha mawazo ya
watu ya kufikiria kuwa uwezo uliomponya kilema ulikuwa ni wa Petro na
Yohana ambayo haikuwa si kweli. Kama uwezo huu haukuwa wao, muujiza huu
siri yake ni nini? Petro aliendelea kusema hivi;
“Mungu
wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa Baba
zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu ….. Na kwa IMANI KATIKA
JINA LAKE, JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU mtu
huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu
uzima huu mkamilifu mbele zenu ninyi nyote” (Matendo
ya Mitume 3:13 – 16).
Hebu
tafakari maneno haya ya Petro; “Na kwa IMANI
KATIKA JINA LAKE JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU….” Wakina
Petro na Yohana waliweka imani yao katika jina la Yesu Kristo. Walikuwa
na uhakika mioyoni mwao kuwa siri ya miujiza imo katika jina la Yesu
Kristo – ndiyo maana walipomkuta
huyo kilema walimwamuru asimame kwa jina hilo!
Weka
imani yako katika jina la Yesu Kristo ukitaka kuona ishara na miujiza ya
Yesu Kristo maishani mwako na kwa wale unaowahudumia pia. Wakijua hili
wanafunzi wa kwanza wa Yesu Kristo walipokatazwa “wasiseme kabisa wala
kufundisha kwa jina la Yesu” na Anasi kuhani mkuu, waliomba wakasema; “…Basi
sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno
lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ISHARA NA MAAJABU
vifanyike kwa JINA LA MTUMISHI WAKO MTAKATIFU YESU” (Matendo
ya Mitume 4:18,29 – 31)Ni muhimu kuwaeleza na kuwakumbusha watu umuhimu wa kuweka imani zao katika jina la Yesu Kristo wakitaka kuona mkono wa Bwana ukiponya, ukifanya ishara na miujiza.
Nakumbuka
kuna mama mmoja alifika nyumbani kwangu akiwa anaumwa sana toka mkoa
mwingine nje ya mkoa huu wa Arusha ninaokaa.
Baada
ya mahojiano naye nilifahamu ya kuwa ameugua bila kupona kwa muda wa
miaka miwili. Na katika miaka hiyo miwili amezunguka kwa watu mbalimbali
kuombewa bila mafanikio. Alipoona haponi akaenda kwa waganga wa kienyeji
ambako nako hakupona. Alipoona kwa waganga wa kienyeji haponi akaanza
kutafuta watu wamuombee tena.
Katika
mazungumzo hayo nilitambua kuwa anapokwenda kuombewa anaweka imani yake
katika watu wanaomuombea na wala haweki imani yake katika jina la Yesu
Kristo.
Nilifungua
Biblia yangu na nikaanza kuzungumza naye juu ya uweza wa jina la Yesu
Kristo, na umuhimu wa yeye kuweka imani yake katika jina la Yesu Kristo
na siyo kwangu. Mwishoni nikamuuliza kama ameelewa na ikiwa yuko tayari
kwa maombi kwa kulitumia jina la Yesu Kristo.
Yule
mama akajibu akasema; “Ndiyo nipo tayari kwa kuombewa, naamini kwa
jina la Yesu Kristo nitapokea uponyaji”
Mara
nilipoanza kuomba, aliangushwa chini na mapepo yaliyojidhihirisha toka
ndani mwake. Nikayaamuru mapepo hayo yamtoke mama yule kwa JINA LA YESU
KRISTO – na mara hiyo yakamtoka na akawa mzima!
Ugonjwa
uliomsumbua kwa muda wa miaka miwili ulitoweka, yule mama pamoja na mume
wake aliyemsindikiza waliondoka kwa furaha huku wakimsifu Mungu kwa
matendo makuu aliyowatendea.
Kumbuka
Petro alisema; “… Kwa IMANI katika JINA LAKE (YESU)
, JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU ….”Atakayeliitia jina la Bwana ataponywa :
Nabii
Yoeli alitabiri kuwa; “Na itakuwa ya kwamba
mtu awaye yote ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAPONYWA; kwa kuwa ….
Watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema;”
(Yoeli 2:32).
Mtume Paulo alitilia mkazo utabiri huu aliposema;
“Kwa
maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa
wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, KILA ATAKAYELIITIA
JINA LA BWANA ATAOKOKA
(Warumi 10:12 – 13).
Kila anayeliitia jina la Bwana Yesu kwa imani anaponywa na, anaokoka kwa
kuwa ndani ya jina hili la Yesu Kristo mna uponyaji na wokovu kwa kila
amwaminiye Yesu Kristo.
Lakini
Mtume Paulo anauliza swali muhimu ambalo ni vizuri kulitafakari; anasema;
“Basi wamwitaje yeye wasiyemwamini? Tena
wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? (Warumi
10:14).
Hili
jambo ni kweli. Huwezi kumwita mtu usiyemwamini. Hii ina maana ya kuwa
ikiwa tunataka watu waliitie jina la Yesu ili waokoke na kuponywa
madhaifu yao, inatubidi tuhubiri na kufundisha juu ya Yesu na jina lake.
Ndiyo
maana Bwana Yesu Kristo alimwambia Anania ya kuwa Paulo “ni
chombo kiteule kwangu, ALICHUKUE JINA LANGU, mbele ya Mataifa, na
Wafalme, na wana wa Israeli” (Matendo ya Mitume 9:15).
Biblia
inasema pia kuwa; “Filipo akatelemka akaingia
mji wa Samaria, AKAWAHUBIRI KRISTO. Na makutano kwa nia moja
wakasikiliza maneno yale yaliyosewa na Filipo, walipoyasikia na kuziona
ishara alizokuwa akizifanya kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi
waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na
viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa
katika mji ule” (Matendo ya Mitume 8:5 – 8).
Smithi
Wigglesworth aliyekuwa mhubiri wa huko Uingereza katika miaka ya 1930
aliwahi kushuhudia katika mahubiri yake kuwa siku moja aliitwa kwenda
kumuombea mgonjwa mmoja wa kifafa aliyekuwa amezidiwa hata kushindwa
kuamka.
Anasema
watu wa eneo lile na hata ndugu zake yule mgonjwa walikuwa wamekata
tamaa. Waliona ndugu yao atakufa kwa ugonjwa huo. Kwa hiyo ilimchukua
muda Bwana Smith Wigglesworth kupata walio tayari kushirikiana naye
katika kumuombea mgonjwa yule.
Mwishoni
alifanikiwa kuwapata, na anasema walikizunguka kitanda cha yule mgonjwa
na wakaanza kuliitia jina la Yesu kwa pamoja wakisema “Yesu, Yesu,
Yesu, Yesu,….” Kwa kulirudiaruda jina hili. Baada ya kuliitia jina
la Yesu kwa muda hivi, anasema nguvu za Mungu zilishuka kitandani kwa
yule mgonjwa, zikamtingisha mgonjwa na kitanda chake.
Yule mgonjwa akapona saa ile ile, akavaa nguo na kutoka nje. Kijiji
kizima kilitaharuki na kushangaa kilipomuona mtu yule amepona. Smith
Wigglesworth alipoona watu wamekusanyika hivyo wakishangaa, alichukua
Biblia yake akahubiri, na watu wengi walikata shauri na kuokoka siku ile.
Ni
muhimu ufahamu ya kuwa muujiza unaofanywa kwa jina la Yesu Kristo
unawavuta watu kwa Yesu Kristo, wamwamini na kumfuata.
Ndiyo maana imeandikwa juu ya Yesu Kristo kuwa;“Hata (Yesu Kristo) alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi WALIIAMINI JINA LAKE, walipoziona ishara zake alizozifanya” (Yohana 2; 23).
Siku
moja nilikuwa katika sehemu fulani nikifundisha juu ya jina la Yesu
Kristo. Mwisho wa somo nilisema watu wanaotaka kujazwa na Roho Mtakatifu
na wanene kwa lugha mpya pamoja na wagonjwa waje mbele. Watu wengi
walikuja mbele.
Niliwaambia
hatutaomba neno lolote zaidi ya kuliitia jina la Yesu kwa pamoja na kwa
kulirudiarudia. Kwa pamoja tukaanza kuliitia jina la Yesu tukisema kwa
sauti; “Yesu, Yesu, Yesu, Yesu…..”
Muda
haukupita mwingi, tukiwa bado tunaliitia jina hili nikasikia toka upande
wangu wa kushoto sauti ya maji mengi yakiporomoka. Nilijua hii ni ishara
ya uwepo wa Roho Mtakatifu kwani mahali tulipokuwapo hapakuwa na mto
wowote karibu, wala mvua ilikuwa hainyeshi. Baadaye nilipowaeleza watu
juu ya sauti hiyo ya maji, kuna wengine pia waliosema kuwa waliisikia.
Tulipoendelea
kuliitia jina la Yesu Kristo, wagonjwa walipona, waliokuwa na mapepo
walipona, na wengine walijazwa Roho Mtakatifu na wakazungumza kwa lugha
mpya. Ishara na miujiza mingi ilifanyika kwa kuliitia jina la Yesu
Kristo.
Kumbuka
Yesu Kristo alisemal “Na ishara hizi
zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa
lugha mpya…” (Marko 16:17 –18).
Hukumu
kwa kutoliamini jina la Yesu
:
“Amwaminiye
yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu HAKULIAMINI
jina la Mwana pekee wa Mungu” (Yohana 3:18).
Usipoliamini
jina la Mwana pekee wa Mungu – jina la Yesu Kristo ujue umekwisha
kuhukumiwa. Hii ina maana ya kuwa unapoteza wokovu; - unapoteza ushindi;
- unapoteza uzima wa milele; - na pia bado unakaa katika mauti! Hebu
soma na kutafakari mistari ifuatayo ili uone umuhimu wa kuliamini jina
la Yesu Kristo:
“Wapenzi,
mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo,
twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda
yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba TULIAMINI JINA
LA MWANA WAKE YESU KRISTO, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa
amri” (1Yohana
3:21 – 23).
“Bali
wote waliompokea (Yesu Kristo) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa
Mungu, ndio wale WALIAMINIO JINA LAKE”
(Yohana 1:12).
“Kwa
maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku
ndiko kushinda kuushindako ulimwengu; hiyo imani yetu. Mwenye kuushinda
ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa
Mungu? …. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa
milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo
uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi
mambo hayo, ili mjue ya kuwa, mna uzima wa milele, ninyi MNAOLIAMINI
JINA LA MWANA WA MUNGU”
(1Yohana
5:4-5; 11 – 13).
“Wala
hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana JINA jingine
chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Matendo
ya Mitume 4:12) – isipokuwa ni JINA LA YESU KRISTO!
MUHIMU :
Kama
tulivyokwisha kukuandikia katika sura ya tatu ya somo hili – ukitaka
kulitumia jina la Yesu Kristo kihalali na uweze kuona uwezo na mamlaka
yake ni muhimu:
Kwanza:
Uwe mwana wa Mungu kwa kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako kama
Bwana na Mwokozi wako;
Pili:
Uwe mtii ukifuata maagizo ya neno la Kristo katika Roho
Mtakatikfu.
Kuna
watu wengine wanataka kuwa watii kufuata maagizo ya neno la Kristo huku
hawapendi kuokoka. Hawajui utii bila kuokoka ni utii nusu – ukitaka
uone muujiza wa jina la Yesu Kristo katika maisha yako inabidi ufanye
yote mawili – uokoke na utii.
Ikiwa
hujaokoka na unataka uokoke sasa isome sala ifuatayo kwa sauti (ikiwezekena
upige magoti) mahali pa utulivu huku ukiamini ya kuwa Mungu anakusikia:
“Ee
Mungu wangu Mtakatifu. Nimesikia neno lako nami nimeamini. Naomba
unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu yote. Damu
ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yangu, naomba initakase sasa
katika roho yangu, nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu
sasa; Ee Bwana Yesu Kristo nakuomba uingie ndani yangu, uwe Bwana na
Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa kunisamehe dhambi
zangu na Ahsante kwa kuniokoa. Amina”
Ikiwa
umeisema sala hii kwa imani, basi sasa wewe umeokoka na dhambi zako
zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na alivyoandika katika
neno lake. Jina la Yesu Kristo ni halali yako kulitumia!
Ukipenda unaweza kutuandikia kwa anwani iliyo HAPA juu ya uamuzi huu ulioufikia leo wa kuokoka, ili tumshukuru Mungu pamoja na wewe na tuzidi kukuombea; na pia, tunakushauri usome "Hongera kwa Kuokoka" inayopatikana kwa kubonyeza HAPA ili kukusaidia zaidi.
prepared by Meshack Ezekia Kitova
No comments:
Post a Comment