Roho Mtakatifuni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote, anayepatikana kila mahali. Yeye pia anayo nafsi na kwa hiari yake ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu kwa kuzingatia mgawanyo wa majukumu waliyokubaliana yaani nafsi ya Mungu Baba, Mungu Mwana(Yesu) na Mungu Roho Mtakatifu. Kazi/lengo kubwa la ujio wake ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika mapenzi ya Mungu.
Mungu hana namna ya kutawala kwenye ulimwengu wa kimwili bila kuwa na mwili wa damu na nyama, kwa kuwa yeye ni Roho (Yohana 4:24). Hivyo hana budi kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo, ili kutawala na kumuongoza mwanadamu katika mapenzi yake (Yohana14:18, 23, 1Wakorinto 3:16-17, 6:19). Kwa sababu hii ni muhimu sana kwetu kutunza mahusiano yetu na Roho Mtakatifu ili tusimzimishe katika maisha yetu.
Paulo akizungumza na ndugu wa Thesalonike alisema ‘Msimzimishe Roho’ (1Wthesalonike 5:19). Paulo alitoa maonyo haya kwa kuwa alijua, Kumzimisha Roho Mtakatifu, kuna athari mbaya sana kwenye maisha ya mwamini katika kulitumikia kusudi la Mungu na hata maisha yake ya kawaida hapa duniani. Swali la msingi ni, kwa namna gani mtu anaweza kumzimisha Roho Mtakatifu? Ukisoma tafsiri za kiingereza, Biblia ya toleo la GNB katika mstari huu inasema ‘Do not restrain the Holy Spirit’ na toleo la KJV linasema ‘Quench not the Spirit’ (1Th 5:19).
Tafsiri hizi mbili zinapanua zaidi tafsiri ya kumzimisha Roho, katika dhana mbili zifuatazo; moja kumzimisha Roho ina maana ya kumzuia Roho Mtakatifu asitawale na kuongoza maisha yako kwa kukataa msaada wake maishani mwako. Pili, kumzimisha Roho Mtakatifu ina maana ya kuishi katika mazingira ambayo yanamfanya Roho Mtakatifu ashindwe kukusaidia.
Mazingira ambayo Roho Mtakatifu anaweza kuzimishwa;
- Kutokumpa nafasi akusaidie
- Kukosa upendo
- Kuongozwa au kuenenda kwa mwili
- Kutokutii maelekezo yake
- Kukosa ufahamu wa utendaji wake
Pia kuna nyakati katika ibada (sifa, maombi nk), Roho Mtakatifu anaweza akashuka juu ya mtu au watu na akataka kusema jambo, lakini viongozi wa makanisa au vikundi husika wakawazuia hao watu. Kufanya hivyo bila uongozi wa Mungu ni kumzimisha Roho. Mandiko yako wazi kabisa kwamba hatupaswi kutweza unabii (1 Wathesalonike 5:20) na wala hatupaswi kuzuia watu kunena kwa lugha (1Wakorinto 14:39). Zaidi tumeagizwa kujaribu mambo yote, na tulishike lililo jema (1 Wathesalonike 4:21).
Je tutajaribuje mambo yote ikiwa tunawazuia watu Kunena na pia tunatweza unabii? Hofu yangu ni kwamba kwa kuzuia watu kunena na pia kutweza unabii tunaweza tukajikuta tunamzimisha Roho Mtakatifu na kukataa uongozi wake kwenye maisha yetu. Ni vema tukakumbuka kile ambacho Paulo aliwaambia Wakorinto juu ya mambo haya kwamba ‘mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu’ (1 Wakorinto 14:40). Naam na hili lina maana ni vema kwanza ujue utendaji wa Roho Mtakatifu ukoje, ili kuepuka kumzimisha kwa kutokujua utendaji wake.
Pengine yapo mazingira mengine ambayo mtu anaweza akajikuta anamzimisha Roho Mtakatifu. Kumbuka jambo hili kwamba kumzimisha Roho Mtakatifu ni kumzuia asikusaidie, jambo ambalo tafsiri yake ni kukataa uongozi wake kwenye maisha yako. Biblia inasema katika Warumi 8:9 ‘Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo huyo si wake’. Usifanye mchezo na Roho Mungu hakikisha unatunza sana mahusiano mazuri kati yako na yeye kwa kutokumzimisha.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe
No comments:
Post a Comment