Ni muhimu sana kukumbuka kwamba Yesu alikufa pale msalabani kwa sababu kubwa mbili moja ni ili kurejesha mahusiano ya Mungu na mtu kwa lengo la kumsaidia mtu aishi hapa duniani kwa kusudi la Mungu na pili ili tupate wokovu na kisha kuurithi uzima wa milele.
Biblia katika kitabu cha Mathayo 26:53-54 inasema ‘Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?’ Kutokana na andiko hili ni vema tukajifunza kwamba;
- Upendo wake (Yesu) ndio uliomsukuma kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu
- Yesu alikuwa na uwezo wa kuangamiza askari waliokuja kumkamata, lakini hakufanya hivyo ili andiko/kusudi la Mungu lipate kutimizwa.
- Ndani ya ufahamu wa Bwana Yesu kulikuwa na mwanadamu, ndio maana kwa kuangalia ‘future’ ya mwanadamu na kusudi la uumbaji wa Mungu ilimlazimu kupitia njia ngumu ya msalaba ili atupate mimi na wewe.
Katika kuendelea kuonyesha thamani ya kifo cha Yesu pale msalabani Yohana naye aliandika akasema ‘Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ila kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye’ Yohana 3:16-17.
Jambo la muhimu ni kwamba Bwana Yesu hayuko kaburini tena, naam alikufa na kufufuka ili awalete wengi kwenye ufalme wake. Hivyo basi mpenzi msomaji nakusihi usiichezee neema hii, nakusihi usomapo ujumbe huu wewe ambaye hujaokoka, fanya maamuzi ya kuokoka na wewe unayemjua Mungu maanisha katika wokovu wako.
Twaliabudu na kulisifu jina lako wewe uliyeutoa uhai wako kwa ajili yetu ee Bwana.
Ahsante kwa siku njema ya leo ambayo Bwana umeifanya kwa ajili yetu ee Mungu.
Basi ndugu zangu tunapoadhimisha sherehe hizi za pasaka tusiifanye kazi ya Yesu pale msalabani kuwa ni bure, bali kuanzia sasa tusienende kama wamataifa waendavyo bali kama wana wa nuru.
No comments:
Post a Comment