Labels

Wednesday, October 10, 2012

KWA NINI ULIZALIWA AU KUUMBWA?

Mwanzo: 1:26“Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, WAKATAWALE samaki wa baharini na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi”
Katika waraka huu nataka tujifunze juu ya kusudi la wewe kuumbwa na nini ufanye ili uweze kutawala.    Zipo sababu nyingi za wewe kuumbwa lakini moja wapo na kubwa ni ili wewe uweze kutawala. Dhana ya  utawala ni pana, mimi nimeigawanya katika nyanja za kiroho, kidini, kisiasa, kiuchumi, ki-ardhi, kibiashara, ki-taaluma nk.
Sasa aina ya utawala ninayotaka kuzungumza ni utawala katika nyanja ya siasa inayopelekea utawala katika serikali. Yafuatayo ni mambo ya msingi ambayo yatakusaidia wewe uweze kutawala sawasawa na kusudi la Mungu la kukuumba;
(a)Kwanza amini kwamba wewe unaweza kuwa kiongozi mzuri na pia siku moja utakuja kuwa kiongozi mzuri  katika serikali ya nchi yako. Amini kwamba hauna upako wa kupiga kura tu, bali pia tayari Mungu ameshakupaka mafuta (upako) wa kupigiwa kura na wakati ukifika wapiga kura watathibitisha hilo.
(b) Pili, amini kwamba inawezekana kabisa kuokoka na wakati huohuo ukawa mwanasiasa na kiongozi mzuri wa taifa lako. Jifunze kutoka kwa wafalme mbalimbali katika Biblia kama vile Daudi, Yehoshfati nk. Siasa sio mchezo mchafu kama wengi wanavyofikiri, shida ipo kwa wale waliojiingiza kwenye siasa. Kama wanasiasa unawaona kama hawafai kwa kuwa ni waongo, au wala rushwa haina maana siasa ni mbaya.
(c)Fanya maamuzi ya kujiunga na chama chochote chenye sera nzuri katika nyanja zote za msingi na hasa kiuchumi. Nakushauri kabla hujajiunga na chama chochote, soma kwanza sera zao, uzielewe na kuzipima vizuri na kisha sasa amua kujiunga na chama hicho baada ya kuwa umeridhika na kuamini kwamba unaweza fanya nao kazi.
(d)Gombea kila aina ya uongozi katika chama chako kwa nafasi zake mbalimbali.
Kuanzia chini mpaka nafasi ya juu. Chukua fomu za uongozi, jaza bila kuwa na shaka, mwombe  Mungu akufanikishe, usiogope kushindwa katika uchaguzi, hayo ni matokeo na haina maana kwamba haufai, huenda sio wakati wa Bwana lakini pia kama kuna makosa uliyofanya jirekebishe
(e)Jenga mahusiano mazuri na makundi mengine katika jamii.
 Usiwabague watu kwa rangi, umri, kabila wala dini zao. Maana hao watu kwanza ndio utakaowaongoza ukipita, wao ndio watakaokupigia kura na zaidi baadhi
yao utafanya nao kazi katika ofisi moja.
(f)Mwisho ongeza ufahamu na Imani yako kuhusu siasa/uongozi. Nenda kwenye Biblia soma mistari yote inayohusu mambo ya utawala na uongozi ili uongozeke kiimani na pia zaidi ya hapo pia ongeza elimu ya dunia hii kuhusu mambo ya siasa.
Naamini ujumbe huu mfupi utakubadilisha kufikiri kwako kuhusu utawala (siasa) na kisha utayafuatilia mambo ya uongozi kwa karibu, hii ikiwa ni pamoja na kujiunga na chama chochote cha kisiasa hapa nchini.

No comments: