Labels

Monday, October 8, 2012

Kusifu na Kuabudu

Bwana asifiwe, mpendwa katika Bwana!
Napenda kukupa mambo machache kuhusu Kusifu na Kuabudu, ingawa nitalenga zaidi Kuabudu. Sababu inayonifanya niseme zaidi kuhusu Kuabudu ni kwa sababu kusifu na kuabudu ni safari inayoanza kutokea nje kwenda ndani. Kwa sababu hiyo kujua Kusifu bila kujua kuabudu ni sawa na kusafiri bila kufika mwisho wa safari.
Nitaanza kwa kuweka andiko. Ninaomba, ukiweza, usisome ujumbe huu kwa haraka bali soma kwa makini huku ukitafuta Mungu akufunulie zaidi. Andiko hili ni Mathayo 6:9 lisemalo, “Basi ninyi salini hivi, Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje” Katika Luka 11 tunapata maneno kama haya ila kwenye mstari wa kwanza inasema kuwa Yesu alikuwa mahali akiomba na baada ya kumaliza mwanafunzi wake mmoja akamwambia, ‘Bwana tufundishe sisi kusali’. Inaonyesha wazi wanafunzi wake walivutiwa na sala za Bwana Yesu. Hapo ndipo Yesu anaanza kuwafundisha.
Watumishi wengi mbali mbali husema jambo ambalo nakubaliana nalo, kuwa huu alioonyesha Yesu ni muundo tu wa maombi au Kusali. Ombi au sala hii ni fupi sana kuwa tu ndiyo Yesu aliyofanya kwenye kufunga siku arobaini au kwenye masaa mengi ambayo Yesu aliomba mara kwa mara, asubuhi pia usiku.  Katika muundo huu wa sala sitaweza kuchukua vipengere vingi ila kimoja kinachohusu sana somo hili.
Yesu alionyesha sala au maombi yanatakiwa yaanze na kulitukuza Jina la Mungu. Kuingia uweponi mwa Bwana kunatakia kuanze kwa kusifu na kuabudu Mungu kisha mambo mengine yanayohusu maombi au sala yaendelee. Mwamini hawezi kuwa mwombaji au muombezi mzuri kama si mwepesi katika sifa na ibada. Tukikosa uangalifu katika hili ni rahisi tukaingia tu kuomba sana ikafika tukawa kama omba omba katika uwepo wa Mungu. Kuwa kila tunapomwendea Mungu tunaomba tu mahitaji yetu. Maombi na maombezi ni ya muhimu ila bila ya roho ya kusifu na kuabudu, maombi yetu yanaweza yajibiwe bila kumjua huyo Mungu anayeyajibu. Nasema hivi kwa sababu kujibiwa maombi na kumjua Mungu ni vitu viwili tofauti.
Watu kumi waliokuwa na ukoma walimlilia Yesu katika kitabu cha Luka 17:13, wakisema Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu”. Hilo lilikuwa ombi lao. Yesu akawaagiza waende kwa makuhani wakajionyeshe huko. Walipokuwa wakielekea huko, wakatakasika, wakapona ukoma uliokuwepo mwilini mwao. Kati yao ni mmoja tu ndiye aliyerudi kuonana na Yesu ili kumjua kibinafsi. Wale tisa walipata jibu la ombi lao bila kumjua mjibu maombi. Sitatenda haki hapa kama sitasisitiza hili kuwa kuna waombaji/waombeaji na wafanya sala wengi ambao kwa kukosa uelewa huu au kukosa kuzingatia jambo hili wameona miujiza mingi na majibu mengi ya maombi bila kumjua Mungu na njia zake. Siri za Mungu hufichuliwa sirini mwa Mungu. Ila majibu tu ya maombi, hata kwa kufunguliwa madirisha ya mbinguni, Mungu anaweza tu kuyashusha. Zaburi 91:1 inasema , “Aketiye mahali pa sirini pake aliye juu atakaa katika uvuli wake Mwenyezi”. Baada ya hilo kutimia, mistari inayofuata inaeleza kuhusu faida zake.
Nitakupa mifano michache kutoka kwenye maandiko ambayo watu waliomba na kupata jibu lakini bado Mungu hakuwa na ukaribu wa kujulikana. Kutoka 3:7, “Bwana akasema, hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko  Misri, nami nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao…..”. Wana wa Israel walimuomba Mungu na akawasikia na kuwaonyesha matendo yake makuu na kuwatoa Misri. La ajabu ni kuwamba miujiza hiyo yote haikuwafanya wamjue Mungu. Waliendelea na uasi mpaka wakafa wote waliotoka Misri wakabakia Musa, Joshua na Caleb ambao ukiwatazama kwa makini utaona wao walimjua Mungu.
Luka 18 inaonyesha mama mmoja ambaye alimwendea kadhi dhalimu katika fumbo ambalo linamaanisha {katika mstari wa kwanza} kuwa watu wanapaswa Kuomba pasipo kukoma. Lakini kuna jambo la ajabu sana katika mstari ule wa saba (7) na nane(8): “Na Mungu je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia atawapatia haki upesi; Walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona Imani duniani?
Nitaomba niishie hapo ili nirudi kwenye Kusifu na Kuabudu. Mungu akupe ufunuo hapo!
Kusifu ni kusema/kuongea au kutangaza sifa za mtu au kitu. Kumsifu Mungu ni kusema, kuongea au kutangaza matendo yake makuu.
Kuabudu ni kuwasiliana na Mungu kwa jinsi ya Yeye ni nani. Ni mawasiliano ya ana kwa ana, kati ya mtu binafsi na Mungu.
Katika kusifu siyo lazima mtu awe anawasiliana na Mungu. Hata kwa kuongea na mtu mwingine,  mtu anaweza akamsifu Mungu. Hata watu wasiomjua Mungu utawasikia mara kwa mara wakimsifu Mungu, kwa kusema ni mkuu kwa kuleta mvua na kadhalika. Lakini kuabudu inahusu mtu binafsi na uso wa Mungu. Kusifu hata kutoka mbali inawezekana, lakini kuabudu ni jambo la ana kwa ana.
Hebu tazama ibada tunazokuwa nazo  kwenye makanisa au mahali pa ibada. Wakati wa Sifa wahusika huwa wengi sana, na hata wasiomjua Mungu hujumuika. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba watu wanapotakiwa Kuabudu, kuingia patakatifu pa patakatifu, wengi hushindwa kuingia kabisa na hata hutamani kipindi hicho kiishe ili watu wafanye jambo jingine. Laiti vipindi hivi vya kuabudu vingekuwa virefu zaidi!
Mambo yote hapa duniani yatakoma: Kuomba, Maombezi, Kuponya wagonjwa, Kuhubiri, Kukemea pepo na kadhalika. Katika mambo ambayo yatadumu milele, mojawapo ni Kumsifu na Kumuabudu Mungu. Kwa nini basi kusifu na kuabudu kuchukuwe muda mfupi zaidi kuliko haya mengine katika ibada zetu?
Viongozi wa Kusifu na Kuabudu.
Ili usichoke acha nije kwenye wapendwa wanaohusika kuongoza vipindi hivi vya kusifu na kuabudu, baadaye nitarudi kumalizia.
1Mambo ya Nyakati 25:1, “Tena Daudi na maakida wa Jeshi wakatenga kwa utumishi baadhi ya wana wa Asafu, na wana Hemani na wa Yeduthuni, watakaotabiri kwa vinubi na vinanda na matoazi…..” Mstari wa 6, “Hao wote waliamriwa na baba yao, waimbe nyumbani mwa Bwana, wakiwa na matoazi, vinanda na vinubi kwa utumishi wa nyumbani mwa Mungu; Asafu, Yeduthuni na Hemani wakiwa wanaamriwa na mfalme”. Sifa na kuabudu wakati wa Daudi, mmoja wa watu waliojua siri ya ibada katika historia, halikuwa jambo la mzaha. Hapo juu tunaona jeshi lilihusika pamoja na mfalme kutenga wahudumu wa kuongoza sifa na kuabudu nyumbani mwa Bwana.
Ili Sifa na Ibada irudi vyema Kanisani au katika kanisa lolote, ni lazima kufanyike mambo  yafuatayo:
1.Wadau kanisani wahusike wote. Hapo juu tumeona serikali iliingilia kati kurudisha sifa na ibada nyumbani mwa Mungu. Lazima watumishi watafute uelewa wa Huduma hii na kuwekeza na kutafuta muda wa kutosha kuwafundisha na kuwafanyia semina viongozi wao wa Sifa na Ibada. Mahali kwingi waimbaji wa sifa wameachwa tu bila kupewa malezi ya kutosha. Wanatakiwa watafutiwe wataalamu wa kiroho na wa muziki, ili wapate uelewa mkubwa zaidi.
2.Viongozi wa Sifa na Ibada wajuwe kuwa kusifu na kuabudu si muziki na muziki sio kusifu na kuabudu. Wadau wengi wa kusifu na kuabudu wanafanya kosa hili na hivyo kukosea. Kusifu na kuabudu ni kitu kinachotakiwa kufanyika maishani mwetu kila mara, kuwe ama kusiwe na muziki! Viongozi wengi wa kusifu na kuabudu huwa wanaanza kuabudu wakija tu kanisani, wanapokuja kwenye mazoezi au wanapoanza kuongoza kipindi. Kiongozi wa kusifu na kuabudu anatakiwa ajae sifa na ibada katika maisha yake. Akisimama mbele ya watu aendeleze jambo ambalo analifanya mara kwa mara kwa mara katika maisha yake ya binafsi.
3.Kiongozi wa Sifa na Ibada ajue aina ya nyimbo zake. Mwimbaji wa nyimbo za kawaida kama za maadili na mwimbaji wa Sifa na Ibada wako tofauti. Kiongozi wa Kusifu na Kuabudu anatakiwa ajifunze kuimba nyimbo za Sifa na Kuabudu. Kuimba, kwa mfano, wimbo wa Daudi na Goliati kwa juma zima haitasaidia sana anapofikia wakati wa kuifanya huduma yake. Anatakiwa ajifunze na aweke nyimbo za Sifa na Ibada moyoni mwake.
4.Viongozi wa Kusifu na Kuabudu wachukuwe Huduma yao kwa mzigo (seriously). Sioni kwa nini mchungaji afunge na aamke saa tisa alfajiri ili kujiandaa kwa ajili ya kufanya huduma ya jumapili halafu wanaaomtangulia madhabahuni waamke saa mbili asubuhi! Kwa kutokujua uzito wa huduma yao, huduma ya kuongoza Sifa na Ibada imedharauliwa na wengi wamejikuta wakianguka kirahisi kutoka kwenye Huduma hii.
5.Viongozi wa Kusifu na Kuabudu wajilinde na kiburi. Ni heshima kumtumikia Mungu katika huduma yoyote na hivyo hakuna sifa zaidi katika kuongoza kusifu na kuabudu! Siku moja kiongozi wangu katika Kusifu na Kuabudu anayeitwa Lindh alimpata mtu anayetaka kujiunga na kikundi cha Kusifu na Kuabudu, akamuuliza kwa nini alitaka kujiunga na sisi, yule mtu alijibu “Nilikuwa shemasi na sasa naona Mungu anataka kuniinua”. Yule ndugu hakuruhusiwa kuingia kwenye kikundi cha Kusifu na Kuabudu kwa sababu hakujua anachotakiwa kufanya.
Mpendwa siwezi kuyasema yote ila napenda kukupa tu muhtasari wangu.
Yohana 4:23, “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu”.
Labda mtu anaweza kuuliza, je! Nitajuaje kuwa sasa nimeanza kuwa na roho ya Kusifu na Kuabudu? Mambo yafuatayo yanaweza kusaidia katika kujitambua:
-Kusali kwako kutajaa Kusifu na Kuabudu, sio tu ‘maombi’. Kama unaweza kuomba masaa kumi, angalia ni mangapi kati ya hayo unatumia kusifu, kutukuza, kuabudu na kuliadhimisha jina la Bwana.
-Unaimba nyimbo za aina gani? Asilimia kubwa ya watu hupenda kuimba nyimbo za kujielezea hisia zao. Hapa siko kumpokonya mtu soko katika uimbaji wake au kanda yake. Lakini ni vizuri ukajua kuwa nyimbo zako zinaleta kitu gani katika maisha yako. Nyimbo za maadili ni nzuri lakini ni vizuri sifa zikajaa kinywani mwako maana Mungu hukaa katika Sifa za watu wake. (Zaburi 34:1)
-Huwa unafanya nini kanisani watu wanaposifu na kuabudu? Kama kila kipindi cha Kusifu na Kuabudu kinamchosha na kumkera mtu, basi hajaumbiwa bado roho ya Sifa na Kuabudu. Akichukua hatua nzuri, hiki kitu kitaumbika moyoni mwake.
-Unathaminije uwepo wa Mungu? Mtu anayependa kuabudu uwepo wa Mungu huwa unatembea naye na akishaonja utamu huo, hujaa hofu ya Mungu na hivyo hujitunza ili asiupoteze. Sijasema nguvu na upako, ila uwepo wa Mungu. Daudi ambaye alikuwa anaabudu sana alilia na kusema, katika Zaburi 51:11, “Usinitenge na uso wako, wala Roho yako mtakatifu, usiniondolee”. Musa naye akasema, katika kutoka 33:15, “….. uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa”. Ni jambo la ajabu Musa kuliomba baada ya miujiza yote ambayo Mungu aliwaonyesha wana wa Israel, na yeye mwenyewe akiwemo. Lakini alitaka uwepo wa Mungu binafsi, siyo tu matendo. Kuna utamu wa ajabu katika uwepo wa Mungu.
Na mwisho kabisa mpendwa, kuwa mwanafunzi wa kitabu cha Zaburi, ambacho Mungu kwa hekima yake alikiweka katikati kabisa mwa Biblia. Kitabu cha Zaburi kina maneno mengi ambayo ni njia mojawapo ya kupata lugha ya kumwabudu Mungu.
Basi, Mungu akipenda tutakuwa pamoja tena. Ubarikiwe sana!

No comments: