na
Meshack Ezekia Kitova
Pamoja na ukweli huu wa sifa na kuabudu kuwa sehemu ya maisha ya mtu ya kila
siku, bado kuna nguvu za ajabu pale waamini wanapomwimbia Mungu sifa. Huduma ya
kumwimbia Mungu nyimbo za sifa na kuabudu, ndiyo huduma pekee ambayo mwamini
hutumia nguvu na bidii nyingi, kupitia nafsi zake tatu. Kwanza, kupitia uimbaji
mwamini hutumia nguvu kumpazia Mungu sauti yake, pili, hutumia viungo vya mwili
wake kama vile mikono, miguu katika kucheza mbele za Mungu wa utukufu. Hali
kadhalika katika kumwimbia Mungu sifa na kumwabudu, mwamini hutumia pia ufahamu
kujihudhurisha mbele za Mungu mwenye maarifa yote. Bidii hizi zinazohusisha
nafsi zote za mwanadamu, ndizo hatimaye zinazomleta mwamini karibu zaidi na
nguvu na uwepo wa Mungu.
Katika kumsifu na kumwabudu Mungu, kanisa la Maranatha Reconciliation
linaelewa kuwa, Roho Mtakatifu aliyemwagwa bila kipimo wakati wa Pentekoste ya
kwanza baada ya ufufuko wa Bwana ni Roho wa sifa. Kiu yake kila wakati ni
kuwaongoza waamini kumtolea Mungu sadaka ya sifa; mahali popote wanapokuwa ikiwa
ni nyumbani, njiani, makazini, vitandani, kwenye maombi, wakati wa ibada n.k.
Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa mafundisho ya kutosha waamini wengi
wameridhika na sifa na kuabudu kunakofanyika katika mikusanyiko ya ibada peke
yake. Wakati umefika kwa watoto wa Mungu kuondoa vifusi vilivyoiangukia huduma
hii na kuifanya ipoteze maana yake ya awali. Vifusi hivi vikishaondoka, kila
mwamini katika nyumba ya Mungu atatambua kuwa, kusifu na kuabudu ni maisha na
sio kuimba peke yake.
Hali kadhalika vifusi hivi vikishaondoka, waamini watatambua pia uhusiano
uliopo kati ya kusifu na kumtolea Mungu shukrani. Ukiangalia mashairi ya mfalme
Daudi, utagundua kuwa, nyingi ya Zaburi zake zinaongelea umuhimu wa kumtolea
Mungu dhabihu za shukrani. Kwa mfano, tunapoangalia zaburi ya 116, tunakutana na
shairi lifuatalo, "Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; Na kulitangaza jina
la BWANA." Zab 116:17. Katika kumsogelea Mungu ni sharti dhabihu hii ya
shukrani itangulie kabla ya ile ya sifa na kuabudu. Ni katika hali ya kumtolea
Mungu dhabihu ya shukrani ndipo Roho wa Mungu anapozimiliki nafsi tatu za
mwamini na kumwongoza kumwadhimisha Bwana kwa bubujiko la ajabu, huku akitokwa
na machozi ya furaha. Kutokana na uhusiano uliopo kati ya sifa, kuabudu na
shukrani, ni sahihi kusema kuwa, ibada ya kweli ni lazima iwe na mambo makubwa
matatu, KUABUDU, KUSIFU na KUSHUKURU.
Kwa maneno haya machache, tunayo imani kwa Mungu kuwa ataleta uamsho wa sifa
na kuabudu kwa kweli katika kanisa lake hapa Tanzania. Wakati huu ambao uovu
unaonekana kuimeza dunia, huduma hii ya kusifu na kuabudu kwa kweli, inahitajika
sana katika kanisa. Huduma hii ndiyo itakayoweza kuziangusha ngome hizi za uovu.
Ngome hizi zikishaanguka, ukuaji wa kanisa kitabia, kiidadi na kijiografia nao
utashika kasi tofauti na ilivyo sasa. Mungu akubariki na akupe kiu na bidii ya
kufanya huduma ya kusifu na kuabudu kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku.
KILA MWENYE PUMZI NA AMSIFU BWANA, HALELUYA!
No comments:
Post a Comment