Kuokoka ni jambo ambalo halieleweki vizuri kwa baadhi ya watu katika imani
ya kikristo. Kuna wakristo wanaokataa na pengine kudhihaki kuwa hakuna wokovu duniani na kwamba
wanaoamini katika wokovu wamechanganyikiwa. Aidha utata mwingine katika suala
la kuokoka ni pale ambapo baadhi ya watu wanaoamini kuwa wokovu upo wanapodai
kwamba mtu hawezi kuokoka akiwa hai bali kuokoka ni baada ya kufariki dunia.
Hayo ni mawazo potofu na inasikitisha zaidi inapoonekana kuwa hata baadhi
ya viongozi wa makanisa hawalielewi vizuri suala hili ambalo ni muhimu katika
imani ya kikristo kwani ndiyo sababu hasa iliyomleta Bwana Yesu Kristo duniani,
kuja kuwaokoa watu katika dhambi zao kama yasemavyo maandiko matakatifu kwamba;
“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili
kukubalika kabisa ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye
dhambi.” 1 Timotheo 1:15. Kutoeleweka
vizuri kwa suala hili matokeo yake ni watu kuyumba au kuyumbishwa kiimani, na
hata baadhi ya wanaodhani wanaelewa maana yake wakijikuta wakiwa nje ya ukweli
na hivyo maana nzima ya wokovu kupotoshwa.
Kwa yeyote anayejiita mkristo lakini
anakataa kwamba hakuna wokovu ajue kwamba hana haki ya kujiita mkristo. Kwani Ukristo
siyo kuwa na majina yanayoitwa ya ‘kikristo’ au labda kula baadhi ya vyakula ambavyo imani nyingine
inakataza kula; bali Ukristo ni imani ambayo ni Yesu mwenyewe kama yasemavyo maandiko
kuwa; “Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa
chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati
imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini
iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.” Wagalatia 3:23-25.
Wokovu unapatikana kwa Yesu Kristo pekee kwa kuwa Yeye ndiye njia pekee ya
wokovu. Mlinzi wa gereza walimokuwa wamefungwa Paulo na Sila baada ya
kushuhudia nguvu za Mungu aliwauliza Paulo na Sila afanyeje ili aweze kuokoka;
“Kisha akawaleta nje akasema ‘Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate
kuokoka?’ wakamwambia ‘mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako” Mdo. 16:30-31.
Wokovu upo na ni kwaajili ya wanadamu walio hai na si vinginevyo. Biblia
takatifu inafundisha kuhusu wokovu. Yaani maana nzima (main theme) ya Neno la Mungu ni Wokovu. Injili inahubiriwa duniani
kote ili watu wamjue Mungu kisha waokoke, na wokovu unapatikana kabla ya mtu
hajafariki dunia. Bwana Yesu mwenyewe amelielezea suala hilo katika mfano
alioutoa kuhusu maisha ya tajiri na maskini Lazaro ambapo baada ya wote
kufariki, Lazaro alikwenda peponi na yule tajiri alikwenda motoni kulingana na
matendo yao. Kwakuwa walikuwa wakionana wakiwa huko, yule tajiri kutokana na
mateso aliyokuwa akipata aliomba Lazaro
atumwe duniani kuwaeleza ndugu zake tajiri jinsi hali ya mateso makali anayopata
mtu asiyeokoka baada ya kufa kwake ilivyo, hivyo kuwataka ndugu zake hao watubu
dhambi zao wakiwa huko huko duniani kwani hakuna nafasi ya kutubu baada ya kifo.
(Luka 16:19-31).
Wokovu unapatikana wakati mtu akiwa
hai tu kwani baada ya kufa kinachofuata ni hukumu, hakuna uwezekano wa
kuutafuta wokovu ukishakufa kwani maandiko yanasema; “Na kama vile watu walivyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu.”
Waebrania 9:27. Dini zipo duniani ikiwa ni jitihada za wanadamu katika
kumtafuta Mungu ili waokoke na kujiepusha na adhabu ya Mungu, kusingekuwa na
sababu ya watu kupoteza muda wao makanisani na sehemu zingine za ibada kama
kusingekuwa na matarajio ya kupata ujira wa wokovu, ingawa hata hivyo wokovu
siyo dini bali ni imani.
Wokovu ni mpango mahususi wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Mungu alipomuumba
mwanadamu alikusudia kumfanya asife, aendelee kuishi milele na kuwa karibu naye.
Hata hivyo Adamu alipofanya dhambi ya kumwasi Mungu ndipo Mungu alipokasirika
na kumfukuza Adamu katika bustani ya Edeni. Dhambi humtenganisha mwanadamu na
Mungu hivyo alimwambia Adamu kwamba atakufa; “Kwa maana u mavumbi wewe nawe mavumbini utarudi.” Mwanzo 3:19.
Mwanadamu anakufa asipokuwa na Roho wa Mungu lakini akiwa na Roho wa Mungu
kinachokufa ni mwili tu lakini Roho yake haifi. Adamu alipomwasi Mungu ndipo
alipojikuta kwa mara ya kwanza akiwa uchi na akaanza kuwa na hofu; yaani hakuwa
tena na ile Roho wa Mungu iliyomfanya
ajiamini. Wanadamu vizazi kwa vizazi wakaendelea kumwasi na kumkasirisha Mungu.
Kutokana na kukithiri kwa maasi, Mungu akaleta gharika kuu na kuwateketeza wote
isipokuwa Nuhu na familia yake tu, kiburi cha mwanadamu hakikukoma; wakiwa
chini ya kiongozi wao Nimrodi wanadamu wakaazimia kujenga mnara mrefu kwa
matofali ya kuchoma huko Babeli ili wamfikie Mungu. Hata hivyo Mungu
akawasambaratisha. Vilevile akaiteketeza miji ya Sodoma na Gomora kwa moto kutokana
na kukithiri kwa maasi lakini akamsalimisha Lutu na wanawe tu. Hicho ndicho
kiburi cha mwanadamu dhidi ya Mungu.
Ndipo Mungu alipochukizwa na kizazi cha wana wa Israeli akawapa adhabu
kwamba kizazi chao kitakwenda utumwani Misri kwa muda wa miaka mia nne. Baada
ya mateso mengi ya utumwani, wana wa Israeli walimlilia Mungu naye akasikia
kilio chao ndipo alipokumbuka agano lake na Ibrahimu, na Isaka na Yakobo kwamba kizazi chao kitakwenda
utumwani Misri kwa muda wa miaka mia nne na baada ya hapo watarudi katika nchi
yao ya ahadi, akaamua kuwaokoa kutoka utumwani
kupitia kwa Musa na kuwarejesha katika nchi aliyowaahidi mababu zao.
No comments:
Post a Comment