Katika kitabu cha Muhubiri 3:1 Biblia inasema “
Kwa kila jambo kuna
majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”. Hivyo
mwanadamu katika maisha yake hapa chini ya jua kuna vipindi mbalimbali
anavyovipitia hii ni pamoja na kipindi cha uchumba kwa sehemu kubwa ya
watu.
Katika kipindi hiki yapo mambo mengi ambayo wachumba hufanya, mengine ni
mazuri na mengine hayafai kabisa. Na hii yote inatokana hasa na mitazamo au
tafsiri ya uchumba kwa watu husika. Fahamu kwamba tafsiri unayokuwa nayo juu ya
mchumba wako ndiyo inayokuongoza kujenga mahusiano ya aina fulani pamoja
naye.
Lengo la somo hili ni;
Kuongeza ufahamu wa wachumba kuhusu kipindi hiki na Kuwapa vijana maarifa ya
kuwasaidia kuishi kwa nidhamu ya Ki-Mungu katika uchumba wao. Pia ni
kuwafikirisha vijana wanaotarajia kupita katika kipindi hiki mambo ya
kuzingatia. Si wachumba wengi wanajua, Mungu anawataka wafanye nini katika
uchumba wao au kwa lugha nyingine si wachumba wote wanaojua kwa nini kipindi cha
uchumba kipo. Naam katika somo hili tumeandika mambo hayo kinaga ubaga.
Kwa kuwa suala la uchumba ni pana na lina mitazamo mingi, yafuatayo
ni mambo tuliyozingatia katika uandishi wa somo hili;
- Kuna makundi mbalimbali ambayo yana taratibu zao kuhusu mchakato wa mtu
kumpata mke au mume kikiwepo kipindi cha uchumba. Makundi hayo ni pamoja na
makanisa, makabila, familia nk.
- Wachumba wanaweza kutofautiana kwa kiwango cha elimu, uchumi, ufahamu juu ya
mambo mbalimbali, kikabila, umri na hata kwa rangi pia.
- Kuna baadhi ya wachumba hadi kufikia muda wanakubaliana kwamba watakuja
kuishi pamoja walishafahamiana tangu zamani na wengine hawakufahamiana.
- Wachumba wanaweza wakatoka katika madhehebu/makanisa tofauti na hili ni kwa
kuzingatia madhehebu/makanisa mengi yaliyopo.
Lengo letu ni kuandika juu ya
mwongozo wa Neno la Mungu katika
kipindi cha uchumba. kwa lugha nyingine, je Mungu anataka wachumba wafanye nini
katika kipindi chao cha uchumba?. Kumbuka uchumba ni
kipindi/wakati. Basi kama ni wakati jua kabisa kuna baadhi ya mambo ambayo ni
lazima yafanyike, kwani Biblia inasema katika Mhubiri 8:5b
“ Na moyo wa
mwenye hekima hujua wakati na hukumu”, neno hukumu linamaanisha
maamuzi, mambo ya kufanya.
Yafuatayo ni mambo ya msingi kufanya katika kipindi cha
uchumba;
Jambo la kwanza – Mruhusu Roho
Mtakatifu afanyike Bwana wa uchumba wenu
2Wakorinto 3:17
‘Basi Bwana’ ndiye Roho; na alipo Roho wa Bwana, hapo
ndipo penye uhuru’.
Kumbuka Roho Mtakatifu ni msaidizi. Hivyo basi ni vema kumtumia vema hasa
katika nyanja hii ya mahusiano katika kipindi hiki cha uchumba. Ni Roho
Mtakatifu pekee mwenye uwezo wa kukujulisha mambo na siri nyingi kuhusu mchumba
wako hata kama yeye hataki kukueleza. Ukimruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana,
yeye atakuongoza katIka kufanya maombi yanayolenga maeneo ya msingi juu ya huyo
mwenzako. Kila mtu ameumbwa pamoja na mapungufu fulani au kwa lugha nyingine
mapungufu/ udhaifu (weakness) ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Roho Mtakatifu
anapokuwa Bwana wa mahusiano yako yeye atakusaidia kuona madhaifu au mapungufu
ya mwenzako kama kitu cha wewe kujivunia(Strength) kwa maana ya kuona udhaifu wa
mwenzako kama kitu chema na si kibaya.
Kumbuka Paulo katika 2Wakorinto 12:9-10. —‘Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa
furaha nyingi, ….kwa hiyo napendezwa na udhaifu——- maana niwapo dhaifu ndipo
nilipo na nguvu. Hivyo Roho Mtakatifu atabadilisha tafsiri ndani yako za vyote
unavyoona kwa mwenzako huenda juu ya umbile lake, umri wake, macho yake, kabila
lake viwe vitu vya wewe kujivunia. Zaidi Roho Mtakatifu pia atakuongoza katika
maombi yatakayosidia kuuondoa ule udhaifu ambao umekuja si katika mapenzi ya
Mungu, yaani wa kishetani.
Jambo la pili – ni wakati wa
kuweka msingi imara wa uchumba wenu na kufahamiana zaidi.
Hili jambo ni la muhimu kuzingatia. Ni vema wachumba wakatafsiri na kuelewa
vizuri maana ya uchumba. Wachumba wanapaswa kuwa na mipaka fulani katika uchumba
wao na kuwa makini kwa kujilinda na mazingira ya kila namna ambayo yanaweza
yakapelekea wao kuanguka dhambini. Ni vema mkajua kwamba ninyi ni wachumba na si
wanandoa. Na kama ni wachumba basi uchumba una mipaka yake na hamruhusiwi
kufanya mambo ya wanandoa. Mipaka hii iwe kwa habari ya kutembeleana,kupeana
zawadi, mawasiliano (ingawa mnapaswa kuwa makini na lugha mnazotumia pia) nk.
Lengo la kutafsiri misingi ya mahusiano yenu ni kujiwekea mipaka na mazingira
yatakayowasaidia kuishi maisha ya nidhamu, ushuhuda na kumletea Mungu
utukufu.
Sambamba na hili sehemu kubwa ya wachumba huwa wanakuwa hawafamiani vizuri.
Japo wapo baadhi ambao walianza tangu shule za msingi/sekondari/chuo na sasa
wamechumbiana hivyo kwa sehemu wanafahamiana vema. Kwa wale wasiofahamiana vema
huu ni wakati wa kumjua mwenzako vizuri kwa maana ya kabila lake, familia yake,
umri wake, interest zake, matatizo aliyo nayo yeye binafsi au ya kifamilia,
mitazamo yake juu ya mambo mbalimbali kama uchumba, ndoa, maisha, wokovu, neno
la Mungu nk. Huu ni wakati wa kumjua mwenzako kwa njia ya maswali mbalimbali ya
msingi yanayohusu vitu nilivyovitaja hapo juu. Lengo hapa ni kujua
mapungufu/madhaifu(weakness) na mazuri(Strength) za mwenzako ili mjue namna ya
kukabilana na mapungufu na namna ya kuendeleza yaliyo mazuri.
Ni vema pia kuulizana historia zenu za maisha ya nyuma. Kabla ya kuokoka
umepitia katika mifumo gani ya maisha ambayo imechangia kukufanya uwe ulivyo.
Kabla ya kumpata uliye mpata ulikuwa umefuatwa na wangapi na uliwakubalia au la,
na kama uliwakubali kwa nini mliachana, na sasa wako wapi, je bado
wanakufuatilia. Hii itawasaidia sana kujipanga vizuri kimaombi na katika
mahusiano yenu na zaidi itawasaidia kuweza kuchukuliana na kuhifadhiana katika
madhaifu ya kila mmoja.
Mungu anapowaunganisha anakuwa na kusudi maalum. Hivyo jua kwamba huyo mwenzi
uliyepewa umepewa kwa ajili ya kusudi fulani la Mungu. Ni wachumba wachache sana
ambao pindi wanapokutana kila mmoja anakuwa anajua walau kwa sehemu kwa nini
aliumbwa. Sasa ni vema mkae chini mfikiri, nini Mungu anataka kukifanya duniani
kupitia ninyi? Na zaidi angalieni kazi zenu au yale mnayoyasomea, Je mtawezaje
kuliimarisha agano la Bwana kwa pamoja kama mke na mume?.
Hapa maana yetu mnatakiwa kujibu maswali yafuatayo? Je ni kwa nini mlizaliwa?
Je kwa nini Mungu amekuunganisha na huyo uliye naye sasa? Na je kupitia elimu,
bisahara zenu au kazi mlizonazo mtawezaje kuimarisha agano la Bwana?, Kwa
kuzingatia vipawa na uwezo Mungu aliowapa, je ni wapi Mungu anataka kuwapeleka
na kuwafikisha? Kama ndani yenu mna huduma fulani, je ni watu gani ambao Mungu
atataka mshirikiane nao katika huduma hiyo?, je ipi ni nafasi yenu katika mwili
wa Kristo na taifa kwa ujumla? Ni vema zaidi mwanaume akajua wito/ kusudi
aliloitiwa ili pia amshirikishe na mwenzake.
Kufanikiwa kwa hili kunahitaji uwepo muda wa kutosha wa wachumba kukutana ili
kupanga na kuweka mambo yao mbalimbali, na kama ni watu walioko mbali basi suala
la mawasiliano kwa njia mbalimbali kama simu, barua pepe, na barua na hata
zawadi ni la muhimu.
Jambo la tatu- ni wakati wa kulinda wazo la
Mungu hadi litimie.
Siku zote uamuzi wowote unaoufanya una gharama. Naam uchumba pia una gharama
nyingi Sana za kuzikabili kuliko unavyofikiri. Gharama hizo ni pamoja na muda,
pesa, mawasiliano, maombi, uhuru nk. Kumpata mchumba au mwenzi ambaye ni wa
kusudi la Mungu, usidhanie ndio umemaliza. Kama huo uchumba wenu ni wa mapenzi
ya Mungu muwe na hakika mtakutana na vita kubwa sana katika kipindi hicho cha
uchumba na lengo ni kuwatenganisha. Ni lazima mjifunze siku zote kuombeana kwa
kumaanisha maana Shetani naye yupo kazini ili kuvuruga hayo mahusiano.
Kumbuka huyo mwenzi ni agano toka kwa Bwana hivyo unawajibika kumlinda,
kumlinda ni pamoja na kuhakikisha wewe hausabibishi au haufanyiki chanzo cha
ninyi wawili kuanguka dhambini, au ukamwacha na kumsababishia majeraha ya
nafsini na hivyo kuharibu mahusiano yake na Mungu. Wapo watu waliofikia kuharibu
mahusiano yao na Mungu kisa mchumba, saa ya ibada imefika mchumba anasema twende
zetu out bwana, unataka kufanya maombi ya kufunga mchumba anasema kesho
nitakutoa out, inagharimu sana muda wa kuwaza pia kwa ajili yake na familia yake
au mahitaji mbalimbali aliyo nayo.
Zaidi pia uchumba unaweza kukunyima uhuru hata wa kuwa na maongezi na rafiki
zako, maana kuna baadhi ya watu huwa hawataki kuona mchumba wake anaongea au
kucheka na watu wengine, na pia kuna wengine ni wachumba lakini wamewekeana
taratibu ngumu utafikiri wanandoa kabisa na ukweli zinawatesa ila kwa sababu
hataki kumpoteza huyo mchumba wake inabidi avumilie. Jambo tunalosisitiza hapa
ni kwamba, uchumba una gharama nyingi angalia mahusiano yako na Mungu
yasiharibikie hapa.
Jambo la nne- ni wakati wa kupanga malengo na mikakati yenu
ya baadae.
Mithali 29:18a “
Pasipo maono, watu huacha kujizuia’
Hili si jambo ambalo vijana wengi hulipa kipaumbele linavyostahili. Katika
hili ni vema wachumba wafikirie mapema ni aina gani ya maisha ambayo wangependa
kuwa nayo, na pia je ni aina gani ya ndoa wanataka kufunga, tatu je ni wapi
wangependa kuja kuishi kwa maishayaoyote. Haya yatawasaidia wahusika kujipanga
ndani na nje kukabiliana na yaliyo mbeleyao.Kamawanataka kufunga harusi kanisani
basi maana yake wanahitaji kuwa na maandalizi mazuri kifedha, waweke katika muda
kila wanalotaka kuelekea katika harusiyaoili iwasaidie kujiaadaa mapema. Malengo
yoyote yale ambayo mtaweka basi hakikisheni yanatekelezeka, yanafikika,
yanapimika na mnayapangia muda wa utekelezaji.
Mambo zaidi ya kuzingatia katika malengo yenu;
Katika hili ni vizuri wachumba waangalie nafasi yao kifedha imekaaje, na
changamoto zinazowakabili wote kwa pamoja. Je hali yao kifedha inawaruhusu
kuzikabili gharama za maandalizi ya ndoa kwa ujumla. Je hali ya kimaisha ya
kijana wa kiume inamruhusu wakati wowote baada ya kuchumbia aweze kufunga harusi
kama anataka. Je nafasi zao kielimu zikoje, je kama zinatofautiana ni kwa
kiwango gani? Na je tofauti zao kiuchumi na kitaaluma zinaweza kuwa kikwazo kwao
kuoana, au kwa wazazi wao nk. Na je baada ya kuwa wamegundua na kupima uwezo wao
katika hayo mambo mawili, je wanaweza wakasaidianaje ili wafike mahali pazuri
wote wawili.
Vijana wengi wa kiume huwa wanakosea sana hapa, wengi huwa wanasema sitaki
kuchumbia/kuoa mpaka niwe nimesha jikamilisha kiuchumi, niwe angalau na maisha
mazuri. Sisi hatushauri sana dhana hii, ukweli ni muhimu kwa kijana wa kiume
akjikamilisha kwa yale mambo ya msingi. Lakini fahamu kwamba kuna wakati
mwingine kuendelea kwako kiuchumi, au kuvuka kwako kimaisha ni rahisi zaidi pale
unapokuwa na mchumba au ndoa yako. Tunasisitiza tena ni vema wachumba wakae
chini na kufikiri ni kwa namna gani wataendelezana kiuchumi na kitaaluma.
Angalizo, ni vema uwe na uhakika kweli huyo mtu ni wa mapenzi ya Mungu kwa maana
ya kuwa ni wa kwako kweli, maana wapo wachumba ambao wamekuwa wakisaidiana mpaka
kulipiana ada, kupeana mitaji, kununuliana nyumba, magari nk, halafu mwishowe
mmoja anavunja maagano, maumivu yake ni makubwa sana.
Jambo la tano – ni wakati wa
matengenezo na kuzijenga nafsi zenu
Wachumba wengi huwa wanafichana mambo mengi sana wanapokuwa wachumba na
matokeo yake hawayashughulikii mapema na hivyo yanakuja kuwaletea shida kwenye
ndoa. Huenda kabla hujakubaliwa wewe tayari mwenzako alikuwa amesha wakubali
vijana au mabinti wengine kwamba ataolewa nao au kuwaoa. Pia kama ni msichana
huenda ameshawahi kubakwa, au kutokana na masumbufu ya kupata mtu sahihi na
wakati mwingine kuachika mara kwa mara imefika mahali huyo msichana akasema
sitaki kuja tena kuolewa. Zaidi huenda mmoja wenu huko nyuma ameshawahi
kufanya uasherati au zinaa kabla hamjachumbiana. Au kuna mwingine amekuwa
akisumbuliwa na tatizo la harufu, kufanya tendo la ndoa na mapepo nk.
Haya yote na mengine mengi yanayofanana na haya yana athari kubwa sana kiroho
na kimwili kwenu kama wachumba na wanandoa watarajiwa kama hayatashughulikiwa
vema katika kipindi hiki cha uchumba. Licha ya kuwa na athari mambo hayo
yamepelekea nafsi za watu au wachumba wengi kujeruhika. Nafsi inapojeruhiwa
inaharibu ndani ya mtu mfumo wa kufanya maamuzi, mfumo wa utiifu kwa Mungu wake,
mfumo wa kunia na kuhisi pia. Sasa mifumo hii inapoharibika inapelekea watu
kufanya maamuzi ambayo yapo nje ya mapenzi ya Mungu kabisa. Nawajua baadhi yao
ambao wameacha na wokovu, na, wengine wamekata tamaa ya kuolewa, wapo walioamua
kuolewa na mataifa ilimradi ameolewa nk.
Hivyo basi tumieni wakati huu kufanya matengenezo na kujengana nafsi zenu kwa
maana ya kuombeana sana, pili kwa kuongeza ufahamu wenu katika neno la Kristo
hasa maandiko yanayolenga uponyaji katika nafsi zenu, tatu kufuta na kufisha
mapatano/maagano yote ambayo mmoja wenu aliyafanya huko nyuma na watu wengine na
pia kufuta picha za kubakwa na kujenga ufahamu wa mtu aliyeathirika kisaikolojia
kutokana na mambo kama hayo kwa njia ya Damu ya Yesu. Hatua hizi zitawasaidia
kurejesha mifumo iliyoharibika na kuziruhusu nafsi zenu zifanye kazi kama
inavyotakiwa.
Jambo la sita – ni wakati wa
kujua taratibu mbalimbali kuelekea kwenye ndoa
Tumeshasema, kila dhehebu au kabila wana taratibu zao kuhusu uchumba hadi
ndoa. Hivyo ni vema wachumba, wakafuata taratibu ambazo zimewekwa na makanisa
yao hasa zile ambazo zipo katika mapenzi ya Mungu. Lakini pia lazima tukubali
kwamba kuna baadhi ya taratibu za makanisa, makabila na hata madhehebu ambazo
nyingine zipo tu lakini hazitekelezeki na nyingine hazimpendezi Mungu.
Sasa ni vema wachumba wazijue hizo taratibu na wajue je wanaweza kuzitekeleza
au la, na kama hawawezi wafikirie kabisa wanafanyeje. Mfano kuna baadhi ya
makanisa ambayo hayaruhusu mtu wa kwao aoe au kuolewa na mtu wa nje ya dhehebu
hilo. Sasa hii ina maana kama una mchumba wa aina hiyo jipange kujibu maswali ya
wazee wa kanisa na Mchungaji vizuri. Na zaidi kuna baadhi ya makabila na familia
hazitaki uoe au kuolewa na watu nje ya kabila lako, au aliyekuzidi umri kama
wewe ni kijana wa kiume nk. Hivyo ni vema kuzijua hizo taratibu ili mjue
mnajipangaje kukabiliana nazo. Ushauri wetu ni huu kama una uhakika huyo mtu ni
wa kutoka kwa Mungu basi simamia la Bwana maana lipi jema, kumpendeza Mungu au
wanadamu?. Kumbuka Mungu ndiye mwenye ratiba ya kila mmoja wetu.
Suala la kukagua/kupima afya zenu kwa pamoja.
Kwa mazingira ya ulimwengu wa sasa suala la ukimwi limechukua sura mpya na
kuleta mtafaruku ndani ya kanisa hasa kwa vijana wanochumbia kabla ya kupima
afya zao. Siku hizi jambo hili limewafanya wachungaji kuomba sana kwa habari ya
vijana ndani ya kanisa. Sasa kama mlikuwa hamjapima afya zenu mpaka mmechumbiana
basi chukueni hatua mwende kupima. Ni vema wachumba wakapima mapema afya zao ili
jambo hili lisije likawaletea shida baadaye, maana kwa sheria ya nchi yetu
wachungaji hawaruhusiwi kufungisha ndoa kama mmoja wa wahusika ameathirika.
Upimaji wa afya zenu ni wa muhimu kwani, ndani ya makanisa kuna rekodi ya
vijana wengi tu ambao wameshaathirika na huenda si kwa sababu ya zinaa, maana
kwa mujibu wa watu wa afya njia za maambukizi ni nyingi. Kuna wengine wamezaliwa
nao, kwa nia ya kuongezewa damu,kutumia vifaa kama nyembe, sindano nk. Hata
hivyo swali la msingi inabaki kwamba
je, liko tumaini kwa mtu
aliyeathirika kuoa au kuolewa?
Tukueleze hivi, hakuna jambo gumu lolote la kumshinda Bwana, hii ni pamoja na
ukimwi, kama Mungu alimfufua Lazaro, alitenganisha bahari ya Shamu na watu
wakapita, kama Yesu alitembea juu ya maji,
basi naomba ujue kwamba
Ukimwi hauwezi kuzuia kusudi la Mungu hapa duniani kwa wale awapendao
na kwa sababu hiyo tunasema hata kama mtu ana ukimwi na Mungu bado ana kazi naye
hapa duniani, hakika atamponya huo ukimwi na atampa mke au mme.
Faida na lengo la kupima ni hili, hata kama majibu yatatoka mmoja ameathirika
isiwe mwanzo wa ninyi kuachana. Kama mna uhakika Mungu aliwaanganisha huu ndio
wakati wa kurudi mbele za Mungu kwa maombi ya uponyaji na kujipanga zaidi juu ya
hilo.
Jambo la saba – ni wakati wa kuongeza
ufahamu wenu kuhusu nafasi yako kwenye ndoa.
Je umeshawahi kujiuliza ni kwa nini Mungu anakupa mke au mme? Yamkini zipo
sababu nyingi lakini baadhi yake ni; Mungu anakupa mke kama msaidizi, mlinzi, na
pia unapopata mke au mme unakuwa umejipatia kibali kwa Bwana na pia ni kwa
sababu ya zinaa ndio maana unahitaji mwenzi. Hizi ni baadhi ya sababu zilizoko
ndani ya Biblia. Hivyo basi tafuteni wanandoa mnaowaamini na zaidi waliokoka
muwaulize kuhusu wajibu wa kila mmoja kwa nafasi yake kwenye ndoa. Katika
hili baadhi ya makanisa huwa yana utaratibu wake wa nani atahusika na maelekezo
ya aina hii kwa wachumba. Hivyo kama kanisa lako lina utaratibu huo, fuata huo
utaratibu.
Katika ndoa kuna mambo mengi sana ambayo mtatakiwa kufanya, ni vema kufuata
mwongozo na ushauri wa viongozi wenu au wachungaji wenu kuhusu nini mnatakiwa
kufanya katika ndoa yenu. Angalizo hapa ni hili, uwe makini na vyanzo vya
ushauri au mafunzo katika eneo hili ili lisije kuleta madhara baadae. Usitafute
wala kufuata kila ushauri, bali sikiliza pia uongozi wa Mungu ndani yako.
Jambo la nane– Msifanye tendo la ndoa,
maana jambo hili litaharibu mpango wa Mungu na kusudi lake kupitia
ninyi.
Wakati wa uchumba, si wa kufanya mapenzi au kufanya michezo ya mapenzi.
Tunarudia tena ili kuonyesha msisitizo kwamba chonde chonde jamani, uchumba sio
ndoa, maana uchumba unaweza kuvunjika. Hairusiwi kabisa kwa wachumba kufanya
mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa kabla ya ndoa. Kitendo cha Mungu
kukujulisha/kukupa huyo mwenzako kama mke/mume mtarajiwa haina maana mna haki ya
kufanya mambo ya wanandoa. Mungu kukupa huyo mwenzako sasa ni taarifa kwamba
huyu ndugu ndiyo atakuwa mkeo au mmeo na anakupa taarifa sasa ili ujipange
kufanya mambo ya msingi mnayotakiwa kuyafanya katika kipindi cha uchumba.
Kipindi cha uchumba ndicho kipindi ambacho wachumba wengi sana wanavuruga kusudi
la Mungu, na kuharibu maisha yao ya baadae na ndoa yao kwa ujumla.
Ndoa nyingi sasa hivi zina migogoro kwa sababu wakati wa uchumba walidiriki
kufanya tendo la ndoa. Vijana wengi hawajajua kufanya tendo la ndoa kipindi cha
uchumba lina madhara gani kwao na ndio maana wengine wanafanya. Biblia inasema
katika Mithali 6:32
“Aziniye na mwanamke hana akili kabisa, afanya jambo
litakalomwangamiza nafsi yake mwenyewe”. Hata kama ukifanya tendo la
ndoa na mchumba wako ambaye mlibakiza siku moja kufunga harusi, bado
umezini.
Ndani ya nafsi ya mtu kuna akili, hisia, nia na maamuzi. Biblia inaposema
afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake ana maana hii, dhambi hii
inapofanywa, ina haribu mfumo wa utiifu na uamnifu kwa Mungu wako, inapelekea
kukosa usikivu wa rohoni kabisa, ina haribu mfumo wa kufikiri, kunia na kufanya
maamuzi. Na kwa sababu hiyo si rahisi tena kusikia na kutii uongozi wa Roho
Mtakatifu. Kwa watu ambao wamezoea kuwa na mahusiano mazuri na Mungu
watanielewa ninachosema hapa.
Zaidi kuna baadhi ya wachumba kweli hawafanyi tendo la ndoa bali wanafanya
michezo ya mapenzi. Michezo ya mapenzi (Fore play) ni maalum kwa ajili ya
wanandoa, na ni sehemu ya tendo la ndoa. Hivyo kufanya michezo ya mapenzi ni
kufanya mapenzi kwa sababu ile ni sehemu ya mapenzi. Kuna vitu unavichochea,
unaamusha hamu ya mapenzi au unayachochea mapenzi. Biblia inasema katika Mhubiri
2:7 “Nawasihi
, enyi binti za Yerusalemu, kwa paa na kwa ayala wa
porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe.”
Mungu pia anachukia michezo ya mapenzi soma Isaya 57:4-5
“Mnafanya
dhihaka yenu juu ya nani, juu ya nani mmepanua vinywa vyenu, Na kutoa ndimi
zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo; ninyi mnaowasha tamaa zenu kati
ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi….. Wachumba wengi
hawajui haya kwa sababu si makanisa yote yanayofundisha maswala ya mahusiano ya
wachumba kimpana.
Mpaka hapa tunaamini umeshajua hasara za jambo hili na utazijizuia kabisa
kulifanya. Michezo ya mapenzi ni pamoja na kunyonyana ndimi, kushikana sehemu
ambazo zinaamsha ashiki ya mapenzi kama sehemu za siri, matiti, kiuno nk, pamoja
na kuangalia picha za ngono. Katika kipindi ambacho tumemtumikia Mungu kupitia
vijana tumejifunza na kukutana na kesi mbalimbali za aina hii na kuona namna
Shetani anavyovuruga mpango wa Mungu kwa vijana. Mwenye sikio na asikie neno
ambalo Roho wa Bwana awaambia vijana ili kulida kusudi la ndoa.
Ni imani yetu kwamba mambo haya nane yameongeza ufahamu na hivyo kuwa maarifa
ya kutosha kukusaidia kuenenda kwa mapenzi ya Mungu katika kipindi cha
uchumba.
Bwana awabariki